Sio mabadiliko pekee, ni mageuzi ya makusudi pia yanayotarajiwa kushuhudiwa kwa kiwango chake ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kufanyika mabadiliko ya uongozi.

Hali hiyo imejidhihirisha kupitia kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho tawala, Humphrey Polepole aliyoitoa hivi karibuni katika mahojiano na kituo cha Uhuru FM kinachomilikiwa na chama hicho.

Alisema chama hicho kinafanya mageuzi ya makusudi, ajenda ambayo alidai ingawa ilikuwapo toka awali haikupata mtu wa kuisimamia kama alivyoonesha nia Mwenyekiti wa sasa wa chama hicho, Dkt. John Magufuli.

Alisema kuwa mageuzi hayo yameanzia katika idadi ya wajumbe wa Halmashauri Kuu na Kamati Kuu ya chama hicho ambayo iliridhiwa na wajumbe wenyewe. Halmashauri Kuu ilipunguza wajumbe 230 na Kamati Kuu ilipunguza wajumbe 10.

Aliongeza kuwa Chama hicho sasa kinafanya kazi ya kuwatumikia wananchi walio wanyonge dhidi ya watu waliokuwa wakijipatia ukwasi kwa kupiga dili.

“Keki ya Taifa kwa muda mrefu imekuwa ikiliwa na wapiga dili na wahujumu uchumi na kutiririsha kidogo kwa wananchi. Kwa hiyo kuwaondoa kunahitaji uvumilivu,” alisema.

Polepole aliteuliwa kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho akichukua nafasi ya Nape Nnauye. Kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo, Polepole alikuwa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma na baadae kuhamishiwa Wilaya mpya ya Ubungo.

Hupaswi kukosa jibu hili la Lowassa kuhusu hatma ya urafiki wake na Kikwete
PolePole: Tunafanya mageuzi ya makusudi ndani ya CCM