Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole amezungumzia uwezekano wa kufungua dirisha la usajili la chama hicho, endapo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa atataka kujiunga.

Polepole ameiambia Times Fm wiki hii kuwa mchakato wa kumpokea mtu aliyekuwa mwanachama wa chama hicho hufanywa kwa mujibu wa Katiba ya chama na kwamba utataribu huo utazingatiwa.

Alisema kwa kawaida ni lazima watakaa vikao kadhaa kumjadili ili kufahamu kama ujio wake una manufaa yoyote kwenye chama.

“Mwanachama wa CCM aliyehama na kujiunga na chama kingine cha siasa, akitaka kujiunga tena na CCM atapeleka maombi yake kwenye tawi lake analoishi. Atajadiliwa na vikao vinavyohusika, na uamuzi wa mwisho wa kukubaliwa au kukataliwa utafanywa na Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ngazi ya Wilaya,” Polepole alisoma ibara ya 13 (5) ya Katiba ya chama hicho.

Hata hivyo, Polepole alieleza kuwa kutokana na uhalisia, ni rahisi kutabiri kama mtu anayetaka kurejea ndani ya chama hicho atakubaliwa au la.

“Kwa bahati nzuri sisi huwa tuko very predictable (tunabashirika). Kwahiyo kuna watu najua hata wakiomba kujiunga na CCM tutawakataa,” aliongeza.

Miezi kadhaa iliyopita, Lowassa akiwa kwenye mikutano ya kampeni kwenye chaguzi ndogo, alisema kuwa Mwenyekiti wa CCM, Dkt. John Magufuli ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwahi kumtaka arejee ndani ya chama hicho lakini alimjibu, “uamuzi wangu haukuwa wa kubahatisha.”

Lowassa alihama CCM na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo mwaka 2015, ambapo alipewa nafasi ya kugombea urais akiungwa mkono na vyama vya upinzani vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Video: Makundi mawili CCM yampinga Magufuli, Mikoa hii hatari kwa wizi wa magari, Wakulima Korosho kulipwa haraka
Fatma Karume afunguka ndoto ya Urais wa Zanzibar, ‘hakuna wa kunizuia’

Comments

comments