Serikali ya Cameroon imewataka wananchi kuwa watulivu baada ya kutokea maandamano ya kupinga kitendo cha polisi kumuua kwa risasi mtoto wa miaka mitano katika Jiji la Buea.

Waziri wa Ulinzi wa Cameroon, kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo akieleza kuwa askari polisi hakufahamu kama amemshambulia mtoto.

Ameeleza kuwa mwanamke alikuwa anaendesha gari kupita katika eneo lenye kizuizi kwa lengo la ukaguzi, askari walimuomba kusimama ili akaguliwe lakini hakutii amri na kuamua kupita akiendelea na safari yake.

“Kutokana na kitendo hicho cha kutotii sheria bila shuruti, askari wetu alifyatua risasi kadhaa za kumuonya ili asimame lakini aliendelea. Ndipo alipoamua kupiga risasi kadhaa kuelekea kwenye gari,” imeeleza taarifa hiyo.

“Katika purukushani hiyo, mtoto Caro Louise Ndialle mwenye umri wa miaka 5, aliyekuwa kwenye gari hilo alijeruhiwa vibaya kichwani na baadaye alifariki dunia,” iliongeza taarifa hiyo.

Mamia ya watu walijitokeza mtaani wakabeba mwili wa mtoto huyo na kuandamana hadi kwenye ofisi ya Gavana.

Hata hivyo, waandamanaji wanapinga taarifa hiyo wakidai kuwa mwanamke huyo alikataa kuwapa polisi fedha kiasi cha 500 franc (sawa na $0.88), ndipo walipopishana kauli na wakaanza kumfyatulia risasi.

Hivyo, waandamanaji wanatembea wakiwa na 500franc wakionesha hewani, wengine wakiwa na matawi.

Muda huu: Kesi ya Sabaya, mafuriko mahakamani
Simulizi: Nilipomfuma mke wangu na Baunsa