Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limetangaza kuanza operesheni maalumu ya kuwasaka wafanyakazi wote waliojipatia ajira kwa kutumia vyeti bandia.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Simon Sirro alitangaza mpango huo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini humo, baada ya jeshi hilo kuwakamata watu watatu wanaoaminika kuwa vinara wa kutengeneza vyetu bandia.

Vyeti Feki

Watu hao walikamatwa katika eneo la Buguruni jijini humo pamoja na mitambo waliyokuwa wanatumia kuzalishia vyeti hivyo vya kuanzia ngazi ya darasa hadi elimu ya juu, pamoja na vyetu vya uuguzi. Jeshi hilo pia lilikamata baadhi ya vyeti vilivyokuwa vinaandaliwa.

Kamanda Sirro alisema kuwa watu hao wametoa ushirikiano kwa Jeshi hilo na wameahidi kutoa taarifa za wateja wao wote. Hivyo, jeshi hilo litazitumia taarifa hizo kuwakamata watu hao.

“Watatutajia kila mmoja mmoja tutawafuata huko waliko. Kama uko Polisi, kama uko ualimu, kama uko hazina, kama uko idara yoyote ya Serikali tutakufuata. Kwasababu bahati nzuri umesema wameanza kazi hii muda mrefu na wana details za kila mtu ambaye amewahi kununua kwao,” alisema Kamanda Sirro.

Mbali na vyeti vya shule na vyuo mbalimbali, Kamanda Sirro amesema watu hao pia walikutwa na leseni za biashara, stika za bima za magari, mitambo ya vivuli bandia vya vyeti vya Chuo cha Biashara (CBE), pamoja na mihuri ya ofisi mbalimbali za Serikali na watu binafsi.

Video: Samia, Majaliwa Wawafunda Wakurugenzi
Juventus Waipotezea Chelsea, Kufanya Biashara Na Man City