Jeshi la Polisi mkoani Njombe, limesema kuwa vitendo vinavyoendelea kutokea mkoani humo vya utekaji, kujeruhi na mauaji vilivyoibuka hivi karibuni vinatokana na imani za kishirikina kwa asilimia kubwa.

Hayo yamesemwa na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Njombe, Rashid Ngonyani alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo amesema kuwa matukio hayo kwasasa yameshamiri zaidi mkoani humo huku wahanga wa matukio hayo wakiwa ni watoto.

Ameyataja matukio yaliyoshamiri mkoani humo kuwa ni pamoja na kunyongwa mtoto wa kike Disemba 2018 katika eneo la Mfereke mjini Njombe, Kujeruhiwa kwa kukatwa koromeo mtoto ambaye jina lake halikufahamika tukio lililotokea Disemba 27 mwaka 2018 katika eneo la Kanisa la KKKT Mji mwema kisha mtoto huyo aliokolewa na wasamalia wema.

Aidha, ametaja tukio jingine ni la mauaji ya mtoto wa kiume, Godluck Mfugale aliyekuwa na umri wa miaka mitano ambaye alitoweka nyumbani katika mazingira ya kutatanisha tangu January 4 mwaka huu kisha mwili wake uliokotwa january 11 mwaka 2019 katika eneo la shule ya Sekondari Njombe ukiwa umeharibika.

“Ndg. Waandishi wa habari sisi jeshi la polisi tunatoa wito kwa jamii pamoja na wazazi wa watoto wanaosoma katika shule mbalimbali hasa za msingi mkoani hapa kuhakikisha wanakuwa makini na watoto wao waepuke kuwasafirisha katika vyombo vya usafiri wa kupewa lifti kwa watu wasiowajua kwakuwa usafiri huo kwasasa hauaminiki, pia wajitahidi kuwapeleka watoto wao shuleni na kuwafuata wakati wa kurudi majumbani,”amesema Kamanda Ngonyani.

Hata hivyo, ameongeza kuwa jeshi la polisi mkoani Njombe mpaka sasa hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kutokana na matukio hayo yote ya ujambazi wa kuteka, kujeruhi na mauaji lakini Jeshi hilo linaendelea na upelelezi wa kina.

 

Video: CAG amjibu Ndugai, anena mazito
Ndugai amlipua Zitto Kabwe, 'Kiongozi muongo sana huyu'