Jeshi la Polisi Mkoani Njombe limefanikiwa kuwaua majambazi wawili kati ya watatu waliokuwa wakijaribu kupora mali kwa kutumia Jambia, Kisu na Panga.

Hayo yamesemwa na Kamanda wa mkoa wa Njombe, ACP Salum Hamduni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa tukio hilo limetokea kijiji cha Lupembe wilayani Njombe aprili 28 majira ya saa 01:40 usiku ambapo watu wasiofahamika walivamia nyumba ya Esau Muhavile kwa kuvunja geti na mlango kwa kutumia Spring ya gari na kuingia ndani kwa nia ya kupora mali.

“Awali majira ya saa 01:30 usiku mlinzi aitwae Linus Matimbwi akiwa lindoni alisikia vishindo vya watu kuzunguka nyumba hiyo na kumgongea Baraka Mayemba mfanyakazi wa Esau na kumweleza kuwa huku nje hali si shwari ndipo Baraka akaamua kumpigia simu mkuu wa kituo kidogo cha polisi Lupembe kwa msaada,”amesema Kamanda Hamduni

Aidha, amesema kuwa Polisi waliwahi kufika katika eneo la tukio na kugundua kuwa majambazi hao wapo ndani na kupiga risasi hewani kuwataarifu kuwa wapo chini ya ulinzi lakini hawakutii amri na matokeo yake jambazi mmoja wapo alirusha jambia na kumjeruhi mkuu wa kituo begani kitendo kilichopelekea Polisi kumpiga Risasi kifuani jambazi Newton Mbanga aliyerusha jambia huku Leonard Alphonce akipigwa risasi kichwani na kusababisha vifo vyao.

“Mbinu iliyotumika na majambazi hao ni kuvunja mlango kwa kutumia spring ya gari na kuingia ndani kwa nia ya kupora mali/pesa na watuhumiwa ambao ni majambazi wawili kati yao walifariki dunia na mmoja alifanikiwa kutoroka, na jeshi la polisi linaendelea kumtafuta mtuhumiwa huyo” ameongeza Kamanda Hamduni.

Marekani: Naibu Mwanasheria Mkuu ajiuzulu, amuandikia Trump ujumbe
Wanne watiwa mbaroni kwa tuhuma za wizi wa Mayai