Jeshi la Polisi mkoa wa Singida limezungumzia tukio la kukamatwa kwa aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu alipokuwa katika Kata ya Itaja, Singida Kaskazini.

Nyalandu na viongozi wengine wawili wa ngazi ya kata wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) walikamatwa jana, Mei 27, 2019 awkiwa katika kata hiyo ambapo taarifa za awali zilidai kuwa alikamatwa na watu wasiojulikana wenye silaha. Lakini baadaye Jeshi la polisi likathibitisha kuwa anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Ni uzushi (sio watu wasiojulikana), amekamatwa na watu wa Takukuru. Watafuteni watu wa Takukuru watawaeleza vizuri ndio waliomkamata,” Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida, Sweetbert Njewike amewaambia waandishi wa habari.

Mkurugenzi wa itifaki na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema alisema kuwa wamepewa taarifa kuwa Nyalandu na wenzake wanashikiliwa na Takukuru kwa tuhuma za rushwa.

“Tumethibitisha kuwa Nyalandu na wanachama wengine wawili wanashikiliwa na Takukuru. Lakini bado hatujafahamu sababu hasa za kukamatwa na Taasisi hiyo,” alisema Mrema.

“Tumewataka viongozi wetu wa Singida Kaskazini kufuatilia kwa karibu suala hilo kwenye ofisi za Takukuru ili kufahamu sababu na mambo mengine, bila shaka watatueleza baada ya kuzungumza na Takukuru,” aliongeza.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Singida, Joshua Msuya amesema kuwa wanamshikilia Nyalandu na wenzake kwa ajili ya kuwahoji kuhusu vitendo vinavyoashiria rushwa na sio kwa sababu walimkuta akitoa rushwa.

“Ni kweli tumemkamata Nyalandu kwa ajili ya kufanya naye mahojiano, kuna mikutano ya kisiasa ambayo wanaifanya na kuna viashiria vya vitendo vya rushwa. Hivyo, tumemkamata kwa ajili ya kumhoji. Tunaomba ifahamike tunamhoji kwa sababu ya kuwepo viashiria vya vitendo vya rushwa na si kwamba tumemkamata akitoa rushwa,” amesema Msuya.

Mkuu huyo wa Takukuru Singida ameeleza kuwa baada ya kumhoji walimkabidhi kwa vyombo vingine vya usalama kwa ajili ya mahojiano zaidi.

LIVE: Yanayojiri Bungeni jijini Dodoma Mei 28, 2019
Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Mei 28, 2019