Mabosi wa Timu ya Polisi Tanzania bado wana matumaini na timu hiyo kusalia Ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuhakikisha inashinda michezo iliyosalia kabla ya msimu huu 2022/23 haujafikia tamati.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Frank Lukwaro amesema bado wana matumani makubwa ya vijana wao kufanya vizuri katika michezo hiyo iliyosalia na kubaki Ligi Kuu ambayo ndio malengo makubwa waliyonayo kwa sasa.

Ameongeza kutokana na msimamo ulivyo, timu nyingi zikipishana alama chache kama Polisi Tanzania itashinda michezo yote mitano ambayo imesalia huku ikiziombea timu zilizo mbele yake kufanya vibaya basi itafikisha alama 34 zitakazo ifanya ibaki.

“Timu inaendelea kufanya maandalizi kuhakikisha inafanya vyema katika michezo yote mitano ambayo ipo mbele yetu, kama uongozi tunapambana kuhakikisha alama 15 tunazichukua.” amesema Lukwaro.

Polisi Tanzania inaburuza mkia katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa na alama 19 iliyopata kwenye michezo 25, ikishinda minne na kuwa timu pekee iliyoshinda michezo michache hadi sasa huku ikipoteza 14 na kutoka sare saba, pia ikiwa imefunga mabao 19 na ikifungwa 35.

Katika michezo mitano iliyonazo, Polisi italazimika kushinda dhidi ya Singida Big Stars Aprili 14 mwaka huu katika Uwanja wa Liti mkoani Singida, kisha itarudi Sheikh Amri Abeid kumenyana na Ihefu FC.

Polisi itaialika Mtibwa Sugar Mei 15 na baadae itakwenda Dar es Salaam kucheza michezo miwili ya mwisho ya ligi dhidi ya Simba SC na Azam FC.

Waziri Mkuu azindua jengo Wagonjwa wa dharula
Wafugaji msiwapeleke watoto kuchunga: ACP Pasua