Maafande wa Polisi Tanzania FC wamesema wataendelea na mfumo wa kuwatumia wachezji wazawa kwenye kikosi chao, kama walivyofanya msimu wa 2019/20 uliofikia tamati jana Jumapili, kwa kushuhudia wakifungwa na Mabingwa Simba SC mabao mawili kwa moja uwanja wa Chuo Cha Ushirika, Moshi-Kilimanjaro.

Polisi Tanzania FC ambao walishiriki Ligi Kuu msimu wa 2019/20 wakitokea ligi daraja la kwanza, ni sehemu ya timu zinazotumia mfumo wa kuwaamini wachezaji wazawa, na wamekua na kiwango kizuri cha ushindani tangu walipoanza mshike mshike wa ligi hiyo mwezi Agosti mwaka jana.

Makamu Mwenyekiti wa Polisi Tanzania FC, Robert Munisi, amesema kuelekea msimu ujao wa Ligi Kuu, uongozi wa klabu hiyo utaendelea kuangalia wazawa na wanaamini nyota wenye vipaji wapo hapa hapa Tanzania.

Munisi amesema watasajili kwa kuzingatia upungufu walioubaini na hawataenda kinyume na mapendekezo yatakayotolewa na benchi la ufundi, linaoongozwa na kocha mzawa Malale Hamsini.

“Hatufikirii wageni, tunaamini wapo wachezaji Watanzania wazuri sana, wakiandaliwa vema wanaweza kushindana na kutupa matokeo mazuri, tuamini vya kwetu, hatufikirii wageni,” amesema kiongozi huyo.

Ameongeza kuwa msimu huu ulimalizika jana, kikosi chao kimefanya vyema na uongozi umewapongeza wachezaji kwa kujituma katika kila mchezo waliocheza iwe nyumbani au ugenini.

“Kwetu mechi ngumu zilikuwa ni Kanda ya Ziwa, Kule tuliteseka, pia hatukuwa na ratiba nzuri, kwa mfano Mbeya tumeenda mara mbili, hii ilitusumbua, mwisho wa yote tunamshukuru Mungu tumeonyesha uwezo wetu,” Munisi alisema.

Polisi Tanzania FC na Namungo FC ya Lindi zilipanda daraja msimu uliopita na kuonyesha ushindani kwenye Ligi Kuu Bara kwa kuzisumbua vigogo wa soka nchini.

Picha: Spika Ndugai na viongozi wengine walivyofika nyumbani kwa Mkapa
China: Ubalozi mdogo wa Marekeni wafungwa