Maafande wa Polisi Tanzania FC wamethibitisha kupeleka mchezo wao dhidi ya Young Africans jijini Arusha katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

Maamuzi hayo yamekuja, kufuatia Uwanja wao wa nyumbani Ushirika uliopo mjini Moshi kuwa na matumizi mengine siku moja kabla ya mchezo huo kupigwa Jumapili (Januari 23.

Jumamosi (Januari 22) kutakuwa na tamasha la Utamaduni uwanjani hapo Mkoa wa Kilimanjaro ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Makamu mwenyekiti wa Polisi Tanzania FC, Robert Munisi amesema awali walipanga kutumia uwanja wao wa nyumbani wa Ushirika katika mchezo huo lakini baada ya kuona itatumika kwenye matamasha la Utamaduni wameona wahamie Arusha ambapo itatoa urahisi kwa wapenzi wao kujitokeza kwa wingi na kuisapoti timu.

Amesema athari za kuhamishia mchezo huo jijini Arusha kutoka Moshi ni kubwa sana kwa sababu Ushirika ni uwanja ambao wameizoea pia maandalizi tayari walishafanya ya kucheza hapo ikiwemo kuboresha sehemu ya kuchezea (pitch), na sasa wanaenda katika uwanja mwingine ambao nao watakuwa kama wageni.

“Katika kanuni mnaulizwa kama ikitokea dharura uwanja wenu wa pili ni upi na sisi uwanja wetu wa pili ni Sheikh Amri Abeid tunakwenda kupambana kushinda hili kubakisha alama tatu nyumbani “

“Tumefanya jitihada zote za kuhakikisha mchezo huo unasogezwa mbele lakini mpaka asubuhi ya leo Alkhamis (Januari 20) jitihada hizo zimeshindikana sasa tunasubiri taarifa rasmi kutoka bodi ya ligi lakini asilimia za kwenda kucheza Arusha ni kubwa” amesema Munisi.

Mara ya mwisho Polisi Tanzania kucheza na Young Africans katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid ilikuwa ni Machi 7 mwaka 2021 ambapo timu hizo zilitoka sare ya kufungana goli 1-1. Bao la Yanga likifungwa na Fiston Abdul Razak dakika 42 huku la Polisi likifungwa na Pius Buswita dakika ya 89.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans ndio vinara kwa alama 32 baada ya michezo 12, imeshinda 10, sare mbili, ikiwa imefunga mabao 22 na kufungwa goli nne pekee, utofauti ya alama 14 na Polisi Tanzania inayoshika nafasi ya nne kwenye msimamo kwa alama 18.

Watu 200,000 hawajui kuwa wameambukizwa VVU
Kibu Denis, Mkude kuikosa Mtibwa Sugar