Jeshi la Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, linamshikilia Frank George mkazi wa kijiji cha Wavuvi, Kurasini kwa tuhuma za kupatikana na magunia 25 ya bangi ikiwa ni tukio la pili ndani ya kipindi cha wiki mbili baada ya jeshi hilo kukamata magunia mengine 24 na kufanya idadi ya magunia 49.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 27,2021, Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Temeke, Amon Kakwale amesema kukamatwa kwa watuhumiwa hao kunatokana na operesheni inayoendelea ambayo inalenga kupambana na wahalifu katika Mkoa huo.

Amesema Februari 25, majira ya saa nne asubuhi walipokea taarifa kutoka kwa msamaria mwema na kwenda kufanya upekuzi kwenye nyumba anayoishi mtuhumiwa huyo na kukuta magunia 25 na puri 208 za bangi.

“Mara baada ya kupata taarifa za kiitelelenjinsia dhidi ya mtuhumiwa huyo anayejihusisha na biashara haramu ya kuuza dawa za kulevya aina ya bangi ndipo timu ya makachero Wilaya ya Chang’ombe  walipoenda kufanya upekuzi,” amesema Kamanda Kakwale.

Aidha, Kamanda Kakwale amesema mtuhumiwa huyo anashikiliwa na jeshi la polisi kwa ajili ya mahojiano na taratibu nyingine za kisheria zitachukuliwa.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 28, 2021
Ahadi ya Balozi Dkt. Bashiru baada ya kiapo