Saa chache baada ya Mo Dewji kuachiwa na watu waliokuwa wamemteka, jeshi la polisi limeeleza jinsi ambavyo bilionea huyo alivyosimulia maisha yake mikononi mwa watesi wake.

Akizungumza mapema asubuhi hii, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa Mo amekiri kuwa waliomteka walikuwa raia wa kigeni waliokuwa wanazungumza lugha moja ya Afrika Kusini.

Amesema kuwa Mo Dewji amesema katika siku zote tisa alizokuwa mikononi mwa watekaji hao, alikuwa amefungwa mikono na miguu pamoja na plasta mdomoni isipokuwa wakati wa kula chakula.

“Walimteka wakampleka kwenye kachumba na godoro, wakamuonesha mahali pa kulala. Lakini kipindi chote hadi anakuja kutupwa [Gymkhana, Posta], siku zote hizi ambazo alikuwa ametekwa, alikuwa ameendelea kufungwa mikono na miguu,” alisema Kamanda Mambosasa.

“Alikuwa anaachiwa tu wakati wa kula, wanamtoa plasta mdomoni na wanamuwezesha kupata chakula. Akishamaliza kula tu wanarudia kumfunga,” aliongeza.

Akizungumzia namna ambavyo walimteka, Kamanda Mambosasa amesema kuwa kwa mujibu wa Mo Dewji, walipomtoa pale Colosseum hoteli jijini Dar es Salaam, Oktoba 11 alfajiri, waliendesha gari kwa mwendo wa dakika 15 wakiwa wamemfunga kitambaa usoni asione anakokwenda na kisha kumfikisha katika chumba hicho kidogo.

Alisema kuwa Mo amepatikana akiwa na afya njema kama alivyoeleza awali msemaji wa familia yake, Azziz Dewji.

Kupatikana kwa 'Mo Dewji' viongozi mbalimbali wafunguka
DNA ya jasho la nguo yamshika mbakaji na muuaji wa watoto

Comments

comments