Jeshi la Polisi limeeleza jinsi lilivyomhoji jana mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu katika Kituo Kikuu cha Jeshi hilo jijini Dar es Salaam.

Kamanda Msaidizi wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Hezron Gymbi amesema kuwa jeshi hilo lilimshikilia na kumhoji Lissu kutokana na madai aliyoyatoa kwenye mitandao ya jamii kuhusu kuwepo kwa kikosi maalum cha jeshi hilo kinachowatesa watuhumiwa.

Alisema jeshi hilo lilimhoji mwanasiasa huyo tangu majira ya saa mbili na nusu asubuhi hadi saa sita mchana.

Gymbi alifafanua kuwa walimtaka Lissu kuthibitisha madai yake kwa kueleza ni wapi kikosi hicho maalum kilipo, na kama ana uthibitisho wowote wa mtu ambaye aliwahi kukamatwa na kuteswa.

Naye mwanasheria wa Lissu, Fred Kihwelu alikiri kuwa aliambata na mteja wake katika Kituo Kikuu cha Polisi jana na kwamba pamoja na mambo mengine, alihojiwa pia kuhusu mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu kupotea kwa msaidizi wa Mwenyekiti wa Chadema, Bernard Saanane.

Katika mkutano na waandishi wa habari wiki iliyopita, Lissu aliwaambia waandishi wa  habari kuwa kabla ya kupotea kwake, Saanane alikuwa akitishiwa maisha na amekuwa akiripoti polisi.

Makonda apiga marufuku bomoabomoa Dar bila kigezo hiki
Nchemba atumia Jamii Forums kutoa ufafanuzi kuhusu kupotea Msaidizi wa Mbowe