Mwanamke mmoja nchini Kenya amesema kuwa amepanga kufungua mashtaka dhidi ya askari wawili wa jeshi la polisi nchini humo kwa kumvua nguo wakidai wanataka kuhakiki jinsia yake kutokana na kuwa na ndevu.

Kwa mujibu wa gazeti la Star, Teresiah Mumbi ambaye anafanya kazi ya udereva na ukondakta wa daladala amesema kuwa alifanyiwa tukio hilo la aibu Mei 15 mwaka huu alipokuwa akishikiliwa katika selo za polisi kwa makosa ya usalama wa barabarani.

Alisema kuwa maafisa hao wa kike walimtoa nje ya selo na kumlazimisha kuvua nguo na kumfanyia tendo la aibu zaidi la kutaka apanue miguu yake.

“Askari wale wawili wakike ambao sikuwatambua majina yao waliponitoa selo na walinilazimisha kuvua nguo na kupanua miguu yangu. Waliporidhika na walichokuwa wanataka walinirejesha tena selo,” alisema Mumbi.

Mumbi amesema kuwa yeye hazinyoi ndevu zake kwakuwa kila anaponyoa hurejea haraka na kuwa nyingi ndani ya siku mbili. Aliongeza kuwa kuzinyoa ndevu hizo humsababishia maumivu.

Mtandao wa Toku umeripoti kuwa Mumbi aliwasihi sana askari hao wa kike kutomdhalilisha lakini waliendelea kumlazimisha kwa madai kuwa wasingetaka kumuweka kwenye selo ambayo sio ya jinsia yake.

Ilani: Picha haihusiani na tukio

Sheria mpya ya faragha yazinduliwa Barani Ulaya
Donald Ngoma atua Azam FC