Katika kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani, Jeshi la Polisi Mkoani Arusha kupitia mtandao wa Polisi wanawake hii leo Machi 8, 2023 wamewakumbuka askari ambao waliumia wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi kwa kwa kuwapa misaada mbalimbali ikiwemo fedha.

Akiongoza zoezi hilo lililofanyika katika Zahanati ya Polisi Arusha, Afisa Mnadhimu wa Jeshi hilo Mkoani Arusha Kamishna Msaidizi wa Polisi, Edith Swebe amesema wameamua kusherehekea siku hiyo kwa kuwakumbuka wateja wa ndani, ni Askari walioumia kazini.

Amesema, mara nyingi huwa wanatoa misaada sehemu mbalimbali ikiwemo vituo vya yatima lakini kwa mwaka huu wakaona ni vyema kuwakumbuka Askari Polisi wagonjwa ambao wamelazwa hospitalini na wengine kuugulia nyumbani.

Aidha, ACP Swebe amebainisha kuwa kupitia maadhimisho hayo pamoja na mambo mengine pia mtandao huo umetoa elimu ya ukatili maeneo mbalimbali ikiwemo shuleni, hospitalini, stendi za mabasi na katika jamii kwa lengo la kukomesha vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.

Akiongea kwa niaba ya Askari waliopewa msaada huo, Mwanaisha Ramadhani ameushukuru mtandao huo wa Polisi kwa moyo wa upendo na kuwakumbuka wagonjwa, huku Polisi hao wanawake wakiungana na wanawake wengine kusherehekea kilele cha siku ya wanawake kwa kufanya maandamano mitaa mbalimbali ya Jiji la Arusha.

IWD: Uwezeshaji kielimu unavyowapaisha wanawake GGML
Tanzania, Namibia kuimarisha Diplomasia ya Uchumi