Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila amewataka wananchi na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao katika mpaka wa Wilaya ya Muleba na Bukoba Vijijini, kutokubali kutoa pesa wanazotozwa na Askari ili kuvuka mpaka nyakati za jioni.

Chalamila ametoa wito huo kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu madai hayo ambapo amesema atafuatilia ili kupata ukweli huku wananchi wakihoji uhalali wa Polisi kuwatoza pesa hizo na matumizi yake.

“Hebu niambie tena naomba urudie ipoje hii umesema ni Polisi kwamba wanakwenda pale mpakani halafu inakuwaje?,” alihoji Mkuu huyo wa mkoa kwa mwananchi ambaye alikuwa akiuliza swali kwake ili kupata ufafanuzi.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Albert Chalamila akiongea mbele ya umati baada ya Mwananchi ()Pichani kulia) kumfikishia malalamiko ya Polisi wanaowatoza shilingi elfu 10 ili kuvuka mpaka.

Akijibu hoja hiyo, Mwananchi huyo alimueleza Mkuu wa Mkoa kuwa, “Ndiyo ni Polisi, wamevaa mavazi ya Polisi wanakuja na gari la Polisi na wana gari limeandikwa Polisi na kama unajua unakwenda pale mpakani imepita saa kumi na mbili uandae elfu kumi.”

Amezidi kufafanua kuwa, “Na ukiwa huna elfu kumi uchague mawili kusimamishwa ili ukope kwa watu na utoke sasa tunashangaa je tunatakiwa wa Wilaya ya Muleba tubaki muleba na wabukoba Vijijini wabaki huko kuna ‘question mark’ hapo.”

Akijibu hoja hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa amesema, “Polisi akikutaka utoe elfu kumi mwambie hivi naomba nimpigie Mkuu wa Mkoa anirushie na niwaambie Askari nawaona mpo hapa haya malalamiko sio mema, Polisi hapokei ushuru wa Halmashauri.

Malalamiko yakitolewa mbele ya halaiki iliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Katika lalamiko la pili wananchi hao wa Kemondo Kagera pia wamemtuhumu mtu mmoja waliyemtaja kwa jina la Ashraf Mzinga, kuwapokonya Samaki na nyavu zao za kuvulia na kusema anafanya hivyo huku wakiwa hawamtambui cheoa chake.

Baada ya lalamiko hilo, Chalamila aliuliza umati endapo mtu huyo yupo eneo hilo, na baada ya kukosekana aliliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta ili aweze kuhojiwa na kutoa maelezo ya yeye ni nani na anafanya hayo kwa maagizo toka ofisi ipi.

Amesema, “Mpaka kufikia saa kumi na mbili huyu Ashraf awe amefika kitu cha Polisi atuambie yeye ni nani, ni kweli sheria za uvuvi zipo lakini tuwasaidie hawa wananchi sio kuwakandamiza. ni sawa na mkaa tunazuia watu kukata miti lakini ukija kwa mkuu wa Mkoa kuna mkaa.”

Kenya: Kenyatta asema 'Mungu awabariki'
Upinzani kuandamana kupinga uchaguzi