Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imelitaka Jeshi la Polisi, Kikosi cha Usalama Barabarani kuacha kuziweka hadharani picha za madereva wanaotuhumiwa kukiuka sheria, badala yake liwafikishe mahakamani kwanza.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo Bahame Nyanduga, wakati akifafanua kuhusu kuwaanika katika mitandao ya kijamii madereva wanaokamatwa na trafiki kwa makosa ya usalama barabarani ikiwemo ulevi.
“Mtu yeyote katika hali yeyote na popote alipo ana haki ya utu wake, sheria na taratibu zinasema anastahili kuishi kutokana na sheria ya utu wake”amesema Nyanduga.
Aidha, Nyanduga amesema si vibaya kuwapiga picha watuhumiwa kwaajili ya uchunguzi wa kipolisi na kumbukumbu zao zibaki katika majalada yao badala ya kuweka picha zao mitandaoni kunakosababisha kuwa ni wakosaji ilihali hawajafikishwa mahakamani.
Hata hivyo ameongeza kuwa utaratibu ulioanzishwa na trafiki wa kuwavisha mabango madereva wanaotuhumiwa kukiuka sheria za barabarani ambayo yameandikwa makosa yao na kurushwa kwenye mitandao ya kijamii kabla hawajafikishwa mahakamani sio sahihi.