Jeshi la Polisi limetoa ufafanuzi juu ya video fupi (clip), inayosambaa mitandaoni ikimuonesha Askari Polisi akichukua fedha kwa raia wa kigeni baada ya mazungumzo ambayo yalionyesha ukiukwaji wa maadili ya Jeshi la Polisi.

Akitoa ufafanuzi huo, hii leo September 14, 2022 Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini kamishina msaidizi mwandamizi wa Polisi, SACP David Misime amesema wanao isambaza video hiyo huenda hawakupata mrejesho wa hatua zilizochukuliwa, dhidi ya askari huyo.

Amesema, Video hiyo ni ya tukio lilitokea Mkoa wa Kaskazini Unguja miaka mitano iliyopita, ambapo askari huyo alishtakiwa na ndani ya siku tatu alipatikana na hatia na alifukuzwa kazi huku akisema Polisi itaendelea kuwachukulia hatua kali Askari wote watakaoenda kinyume na maadili ya Jeshi.

Sehemu ya Video inayosambaa mitandaoni ikimuonesha Askari huyo akipokea pesa kutoka kwa Mtalii tukio ambapo Jeshi la Polisi limesema lilifanyika miaka mitano iliyopita.

Kupitia kipande cha video hiyo iliyosambaa, Askari huyo alionekana akiomba na kupokea rushwa ili aweze kumsamehe kosa la kutofunga mkanda katika tukio la kutoelewana na raia huyo wa kigeni aliyeapa kutorudi tena Zanzibar.

“I will never come back to Zanzibar… ever (Sitarudi tena Zanzibar… milele),” alisema raia huyo wa kigeni huku akipoozwa na askari huyo aliyekuwa akiwaelekeza namna ya kuwakwepa askari wenzake huku muda wote mkono wake ukielekea kwenye pesa aliyoiomba.

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Septemba 15, 2022    
Aliyetupa kichanga akidai kukataliwa akamatwa