Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kuwa jeshi la polisi linazo taarifa za watu walioshiriki mauaji ya kiongozi wa (CHADEMA) katika Kata ya Hananasif, Daniel John ambaye aliuawa na watu wasiojulikana.

Ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, ambapo alikuwa akitoa tathimini ya ulinzi na usalama katika kipindi cha uchaguzi wa marudio katika jimbo la Kinondoni ambapo amesema kuwa mpaka sasa wanazo taarifa za watu ambao wameshiriki kufanya mauaji hayo.

“Taarifa bahati nzuri tumeletewa na watoa taarifa wakielezea sakata zima la mauaji haya yalivyofanyika na kwa sababu tayari tunazo taarifa tunaendelea kufuatilia ili kuhakikisha wahusika wanakamatwa ili waweze kuhojiwa na kufikishwa kwenye vyombo vya mahakama kujibu tuhuma ambazo zinaendelea,”amesema Kamanda Mambosasa

Aidha Kamanda Mambosasa amewaomba Watanzania kuwa wavumilivu na kusema kuwa tukio hilo ni tukio la mauaji kama yalivyo mengine hivyo haki itatendeka kwani kwenye taratibu za upelelezi hakuna ‘double standard’ bali zinafuatwa taratibu na miongozo iliyopo kwenye masuala ya upelelezi.

Hata hivyo, Februari 14, 2018 Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe alitoa taarifa juu ya kuuawa kwa kiongozi huyo wa CHADEMA ambaye mwili wake ulikutwa ukiwa na majeraha mbalimbali mwilini.

 

Video: Mbowe asakwa kuhusu kifo cha mwanafunzi
JPM atoa kauli juu ya mwanafunzi aliyepigwa risasi