Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewaita viongozi waandamizi saba wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ikiwa ni pamoja na mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amekiri kuwaita viongozi hao akieleza kuwa uamuzi wa kuwaita ni nafasi ya upendeleo kwani walitakiwa wakamatwe kama watuhumiwa.

“Hao ni watuhumiwa, na kama wameitwa ni privilege (upendeleo) lakini kwa yaliyotokea walipaswa kukamatwa,” Kamanda Mambosasa anakaririwa.

Wito huo umekuja ikiwa ni siku nne tangu mwanafunzi wa NIT, Akwilina Akwiline kupigwa risasi na askari wa polisi katika harakati za kuwatawanya waandamanaji wa Chadema katika eneo la Mkwajuni-Kinondoni jijini Dar es Salaam waliokuwa wanaenda katika ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kufuata barua za utambulisho/kiapo za mawakala wao.

Viongozi hao walitakiwa kufika polisi jana majira ya saa kumi na moja jioni, kwa mujibu wa mkurugenzi wa itifaki, mawasiliano na mambo ya nje wa Chadema, John Mrema.

Aliwataja viongozi hao waliotajwa kwenye barua ya Polisi, pamoja na Mbowe kuwa ni Halima Mdee, John Heche, Salum Mwalimu, Esther Matiku, John Mnyika na Dkt Vicent Mashinji.

Viongozi hao wanatuhumiwa kuratibu maandamano yasiyo na kibali katika eneo hilo la Kinondoni, siku moja kabla ya kufanyika uchaguzi wa ubunge wa Kinondoni.

Nikki wa pili awafunda kinadada, akumbushia enzi za mababu zetu
Akwilina kuagwa chuoni NIT