Heri kwa Wanawake wote Duniani, ambao hii leo Jumatano Machi 8, 2023 wanasherehekea siku yao ya Kimataifa, ambayo pia hujulikana kama International Women Day – IWD, inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa – UN.

Rasmi siku hii iliasisiwa mwaka wa 1908, wakati wanawake 15,000 walipoandamana katika jiji la New York wakidai muda mfupi wa kazi, mishahara bora na haki ya kupiga kura, na kwa mwaka huu (2023), ikiwa na kaulimbiu isemayo, “Uvumbuzi na Teknolojia kwa Usawa wa Jinsia.”

Iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1911, huko Austria, Denmark, Ujerumani na Uswisi na kwa zaidi ya karne moja, dunia nzima imefanya Machi 8 kuwa siku maalumu kwa wanawake huku mwaka huu kitaalam ikisherehekewa kama siku ya 112 ya Kimataifa.

Wanawake, watasherehekea siku hii kwa kutafakari jinsi walivyopiga hatua kijamii, kisiasa, kiuchumi na kujadili changamoto wanazozipitia na jinsi ya kuzikabili na wazo la kuifanya siku hii kuwa ya kimataifa, lilitoka kwa Mwanaharakati wa kikomunisti, Clara Zetkin.

Ilikuwa ni mwaka 1910, alipopendekeza wazo lake kwenye Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake Wanaofanya Kazi huko Copenhagen – Denmark, uliohudhuriwa na wanawake 100 kutoka nchi 17, na kulikubali pendekezo lake kwa kauli moja.

Dar24 Media tunasema, Wanawake wanatakiwa kupewa nafasi sawa na Wanaume katika maeneo ya kazi na muda umefika kuona kuwa mwanamke si kiumbe dhaifu asiyejiweza, bali kutambua kuwa mwanamke ni mtu muhimu katika jamii na anapopewa nafasi, anaweza kufanya mambo makubwa.

Waziri Mkuu azipa Wizara magizo ufugaji wa kisasa
MPC yathibitisha kifo cha Richard Makore, Waandishi wamlilia