Uongozi wa klabu ya Azam FC umesema mshambuliaji wa klabu hiyo kutoka nchini Zimbabwe Prince Mpumelelo Dube haendi popote, licha ya kuhusishwa na taarifa za kunyatiwa na klabu nyingine za Ligi Kuu Tanzania Bara, katika kipindi hiki cha kuelekea mwishoni mwa msimu huu 2020/21.

Dube ambaye ni muhimili mkubwa katika safu ya ushambuliaji ya Azam FC, anatajwa kuwindwa na mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, huku taarifa zikieleza kuwa, huenda uongozi wa klabu hiyo ukaanza mazungumzo na wakala wake.

Afisa mtendaji mkuu Azam FC Abdulkarim Amin ‘Popat’, amesema mshambuliaji huyo ataendelea kuwa sehemu ya kikosi chao kwa mujibu wa mkataba wake, na wanaamini taarifa zinazoendelea kwa sasa zinapikwa makusudi.

“Kwa kifupi Dube hatakwenda popote ndani ya nchi hii, ataendelea kubaki Azam. Kama akiondoka hapa Azam, basi atakwenda kucheza soka nje ya Tanzania na siyo kwenye klabu za hapa”

“Hizo timu zinazomtaka hata watoe dau kubwa kiasi gani, sisi Azam hatutalipokea, hivyo nao waende kutafuta wachezaji bora nje ya nchi kama sisi tulivyokwenda kumtafuta Dube,” amesema Popat.

Mpaka sasa Dube ndio kinara wa ufungaji kwenye orodha ya wafungaji bora Ligi Kuu Tanzania Bara, akifuatiwa na Meddie Kagere na John Rafael Bocco wote wa Simba SC.

Breaking news: Nyalandu arejea CCM baada ya siku 1278
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Aprili 30, 2021