Mamlaka ya udhibiti wa Manunuzi ya umma (PPRA) imeazimia kuzifikisha katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), taasisi tisa za umma zilizobainika kuwa na viashiria vya rushwa kupitia ukaguzi uliofanywa na Mamlaka hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2015/16.

Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa bodi ya PPRA, Balozi Martern Lumbanga alizitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na Ofisi ya Bunge, Mamlala ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Wakala wa Nishati vijijini (REA), Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Makumbusho ya Taifa, Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (DART) na Wizara ya Maji ya Umwagiliaji.

Balozi Lumbanga alisema kuwa ukaguzi huo ulibaini viashiria vya rushwa katika taasisi hizo tisa kupitia miradi 20 iliyokuwa ikitekelezwa na taasisi hizo.

“Taasisi hizi zilipimwa na kupata asilimia 20 au zaidi katika viashiria vya rushwa hivyo viliashiria uwezekano wa kuwepo kwa vitendo vya rushwa,” alisema Balozi Lumbanga. “Hata hivyo, ieleweke kwamba viashiria vya rushwa hivyo pekee sio uthibitisho kamili wa kuwepo kwa vitendo vya rushwa. Ndio sababu tunawapa Takukuru ambao wao wana mamlaka ya kufanya uchunguzi kupata uhalisia,” aliongeza.

Katika hatua nyingine, Balozi Lumbanga alisema kuwa ukaguzi huo uliofanywa kwa mikataba 21,313 ya manunuzi ya umma yenye thamani ya shilingi trilioni 1.05 ulibaini kuwa serikali ilipata hasara ya shilingi bilioni 23.41 kupitia taasisi za umma kutokana na sababu mbalimbali za kutozingatia kanuni na sheria ya manunuzi ya umma.

Mwenyekiti huyo wa PPRA aliongeza kuwa kwa mwaka wa fedha 2015/16, ilibaini kuwepo kwa malipo yenye utata ya shilingi bilioni 1.3 iliyofanywa na taasisi nne ambazo ni Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, REA, Taasisi ya Mifupa (MOI) na Mfuko wa Pensheni wa LAPF.

“Moja kati ya sababu za malipo hayo kuwa na utata ni taasisi  hizo kuwalipa makandarasi kwa kazi ambazo hazikufanyika,” alisema.

Alisema katika utekelezaji wa majukumu yake, PPRA iliweza kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 852.62 baada ya kufuta michakato ya zabuni mbili, baada ya kujiridhisha kuwa Serikali isingepata thamani halisi ya fedha kama ingetekelezwa.

Aliongeza kuwa iwapo taasisi za umma zitatekeleza mapendekezo ya PPRA, zitaweza kuookoa zaidi ya shilingi bilioni 62.45 za walipa kodi.

“Serikali inaweza kuokoa takribani shilingi bilioni 62.45 endapo taasisi husika zitatekeleza mapendekezo yaliyotolewa na PPRA,” alisema.

Ukaguzi huo pia uliweka wazi taasisi kumi zilizofanya vibaya zaidi katika utekelezaji wa sheria ya manunuzi ya umma kuwa ni Taasisi ya Uzalishaji (NIP), DART, TCRA, Makumbusho ya Taifa, Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, Halmashauri ya jiji la Mwanza, Kampuni ya Reli (TRL), Taasisi ya Mifupa (MOI), Halmashauri ya Manispaa ya Musoma na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka – Bukoba (BUWASA).

 

Chadema watangaza staili mpya ya Ukuta, sasa ni mwendo wa ‘kupaa’
Video: Simba na Yanga watunishiana misuri kuelekea Oktoba 1