Msanii Jackson Kimotho Ngechu almaarufu Prezzo ambaye ni mashuhuri nchini Kenya hususani mwanzoni mwa miaka ya 2000, ametangaza kuwania kiti cha ubunge Kasarani akiwa mgombea huru.

Prezzo ambaye pia amepewa jina la utani ‘King of Bling’ ni mmoja wa wasanii waliotangaza azma ya kujitosa kwenye ulingo wa siasa, katika uchaguzi wa mwezi Agosti 9.

Hata hivyo haijabainika ni kwa nini mwanamuziki huyo alibadilisha nia ya awali, ya kuwania ubunge Kibra na kuhamia Kasarani.

Prezzo alipata afueni kubwa baada ya msajili wa vyama kumuidhinisha kuwa mwaniaji wa kujitegemea, baada ya kuthibitisha kuwa hakuwa amejisajili na chama chochote.

Prezzo atakabiliana kooni na Ronald Karauri ambaye ni CEO wa kampuni ya SportPesa akiwa pia mwaniaji wa kujitegemea na Mbunge wa sasa Mercy Gakuya .

Msanii huyo ameporomosha vibao kadhaa kama vile Hot Step, nataka niwe na wewe, mahangaiko, naleta action na sijakusahau miongoni mwa vibao alivyoangusha.

Rapa huyo mkongwe alitangaza kujitenga na chama cha Wiper kinachoongozwa na Kalonzo Musyoka, mwezi Januari 24 mwaka huu.

Prezzo ambaye alijiunga na chama hicho mwaka 2019, aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa katibu mkuu wa chama hicho.

Mwimbaji huyo hata hivyo, hakufichua sababu yake ya kuondoka katika chama hicho lakini katika ujumbe wake wa awali alisema kuwa atahamia katika chama kingine.

Eng.Hersi Said: Tumerudi kwenye njia ya Ubingwa
Sakata la Deo Kanda, Mtibwa Sugar watinga TFF