Mshambuliaji kutoka nchini Zambabwe na klabu ya Azam FC Prince Mpumelelo Dube, huenda akaukosa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Mabingwa watetezi Simba SC.

Taarifa kutoka Azam FC zinaeleza kuwa kinachomsumbua Mshambuliaji huyo hakijulikani hadi sasa licha ya kufanyiwa vipimo kadhaa. Yaani vipimo havionyeshi kama ana tatizo lolote, lakini mwenyewe analalamikia kuumwa nyonga.

Hali hiyo inamuweka shakani Dube mwenye mabao 14 kuelekea mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba SC, utakaopigwa Azam Complex Chamazi Julai 14.

“Baada ya kuona ana maumivu makali tulimpeleka Hospitali ya Saifee kisha kuchukuliwa vipimo vya (MRI) ila bahati mbaya hakuonekana na tatizo lolote katika mwili wake yaani alionekana yupo kawaida tu,” amesema Daktari wa timu ya Azam, Mwanandi Mwankemwa.

Amesema kwa sasa wanajiandaa kumfanyia vipimo zaidi na kama itashindikana kugundulika tatizo lake watalazimika kumpeleka Mzimbabwe huyo nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

Azam FC inajiandaa kuwa mwenyeji wa mchezo wa Julai 14, huku ikiwa imeshapoteza matumaini ya kutwaa ubingwa, kufuatia kuwa na alama 64 huku ikisaliwa na michezo miwili kabla ya msimu wa 2020/21 haujafikia kikomo baadae mwezi huu.

Simba SC inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 73, huku ikisaliwa na michezo minne kabla ya msimu wa 2020/21 haujafikia kikomo baadae mwezi huu.

Huu ndo mkakati wa kuthaminisha dagaa
Ujenzi wa sanamu la Magufuli viwanja vya sabasaba