Mtayarishaji (producer) nguli wa filamu za Hollywood, Harvey Weinstein amejibu tuhuma zilizoelekezwa kwake na muigizaji wa kike, raia wa Kenya, Lupita Nyong’o kuwa alimnyanyasa kingono.

Lupita alimtuhumu Weinstein kupitia ‘New York Times’ akieleza kuwa alimualika kwake kuangalia filamu, lakini baadae alimlaghai na kumuingiza kwenye chumba chake cha kulala, na kisha kumuweka kitandani kwake akijaribu kutaka kufanya naye mapenzi kwa ahadi ya kumsaidia kufanikiwa kwenye kiwanda cha filamu cha Hollywood.

Weinstein amekanusha madai hayo ya Lupita kupitia muwakilishi wake, ingawa anatuhumiwa na zaidi ya waigizaji wa kike 40 kwa unyanyasaji wa kingono.

“Weinstein ana maelezo tofauti ya matukio, lakini anaamini Lupita ni muigizaji mwenye akili na ana mchango mkubwa kwenye kiwanda hiki. Tuhuma zote za unyanyasaji wa kingono zinapingwa vikali na Bw. Weinstein,” imeeleza taarifa iliyotolewa na mwakilishi wake.

Ameongeza kuwa ni Lupita ndiye aliyemtumia mwaliko akiomba wakutane kwa ajili ya masuala ya filamu na kwamba hakuna matukio yanayohusisha ngono dhidi yao.

Kadhalika, taarifa hiyo ilieleza kuwa tuhuma zote dhidi ya Weinstein zinazotolewa na waigizaji wa kike hazina ukweli wowote.

Weinstein ni mtayarishaji wa filamu za Hollywood mwenye ushawishi mkubwa na anayeshiriki katika utayarishaji wa filamu zenye thamani ya mabilioni ya dola za Kimarekani.

Mtayarishaji huyo wa filamu ni mmiliki mwenza wa kampuni kubwa ya utayarishaji wa filamu ya Miramax ambayo imetayarisha filamu kubwa kama Pulp Fiction, Clerks, The Crying Game, and Sex, Lies, na Videotape.

Amewahi kushinda tuzo kadhaa ikiwemo ya Oscar (Academy Award) kwa kutayarisha filamu ya ‘Shakespeare in Love’.

Wanafunzi 15 wafariki dunia baada ya mlipuko kutokea
M.I wa Nigeria amshtaki Nas kwa utapeli