Nchi za Afrika zimetakiwa kushikamana katika masuala ya maendeleo, biashara na uwekezaji ili kuondokana na utegemezi ili kuliwezesha bara la Afrika kufanya mambo yake kwa uhuru bila kuingiliwa na mataifa mengine ya nje.

Kauli hiyo imetolewa Jijini Dar Es salaam na kiongozi wa Mabalozi wa nchi za Afrika nchini Dkt. Ahamada El Badaoui Mohamed, wakati Mabalozi hao walipokutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi.

Kiongozi huyo ambaye pia ni Balozi wa Visiwa vya Comoro amesema njia pekee ya Afrika kutoingiliwa katika mambo yake ya ndani ni kuhakikisha kuwa bara la Afrika linaweka mikakati madhubuti itakayoliwezesha kujitegemea.

Naye Balozi wa Kenya nchini Dany Kazungu amesema kikao hicho cha mabalozi wa Afrika na Prof. Kabudi hususani katika kipindi hiki cha kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 28, umewawezesha mabalozi hao kufahamu namna Tanzania ilivyojiandaa kutekeleza demokrasia na kuwataka waafrika kujivunia nchi zao na kuwa wazalendo.

Kwa upande wake Prof. Kabudi ameitumia fursa hiyo kuwaeleza Mabalozi hao namna Tanzania inavyoheshimu na kukuza diplomasia na mahusiano baina ya nchi za Afrika, kulinda demokrasia na haki za binadamu, nanamna inavyotumia fedha zake katika kuleta maendeleo ya watu na vitu jambo lililoiwezesha Tanzania kuingia katika nchi za uchumi wa kati kabla ya muda uliotarajiwa.

Mkutano huo umehudhuriwa Mabalozi 15 na wawakilishi wa Balozi 8 walitumia fursa hiyo kumuombea Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Baba wa Taifa hayati Julius Kambarage Nyerere kama Baba wa demokrasia Barani Afrika pamoja na kuuombea uchaguzi mkuu wa Oktoba 28.

Walichosema Kinana, Lowassa kuhusu Magufuli
Anwani za makazi kurahisisha biashara mtandao