Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzania itashirikiana na nchi yoyote duniani, ambayo inatambua na kuheshimu Uhuru wa nchi na utu wa watu wake. 

Prof. Kabudi ametoa kauli wakati akizungumza na watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zake tangu alipoteuliwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuwa Waziri wa Mambo ya Nje. 

“Tutafanya kazi na nchi zote ambazo zinatuheshimu, zinatutambua kama Taifa huru, kutuheshimu sisi kama binadamu wa mataifa mengine, hatutakubali kudharauliwa, kutokuheshimiwa utu wetu na kudharauliwa kwa sababu ya misaada au pesa’, amesema Prof. Kabudi. 

 “Tuko tayari kuwasikiliza na kujadiliana nao kwa heshima na kama wanadhani kuna kitu kimepungua kwetu na sisi tunadhani kimepungua kwao,” ameongeza Prof. Kabudi. 

Prof. Kabudi amesema Tanzania haiwezi kumruhusu mtu yeyote atumie misaada ya fedha kuondoa uhuru wetu na kutokuthamini utu wetu. 

“Hatutajitenga katika dunia hii, tutaendelea kujumuika katika kazi mbalimbali kama vile ulinzi wa amani, kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kuhifadhi mazingira,’ alisema na kuongeza kuwa tumekuwa bandari ya amani kwa wakimbizi sio tu kutoka Afrika bali  duniani kote na tutaendelea kuwa hivyo,” ameongeza Prof. Kabudi. 

Awali akimkaribisha Waziri kuzungumza na watumishi, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wibert Ibuge aliwapongeza watumishi utendaji mzuri wa kazi na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii na uadilifu.

Mahakama Pennsylvania yatupilia mbali madai ya Trump
‘Kivumbi’ baada ya akaunti ya Papa ku-like picha ya 'kimodo', kinachoendelea…