Profesa Ibrahim Lipumba amesema kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa kilichofanyika Zanzibar ni batili kwa kuwa walikiuka katiba ya chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari Septemba 28, 2016 jijini Dar es Salaam, Prof. Lipumba amesema kuwa bado anatambua yeye ni mwenyekiti halali wa chama hicho, kwa kuwa wenye mamlaka ya kumvua madaraka ni Mkutano Mkuu ambao huwashirikisha wajumbe kutoka Bara na Zanzibar.

Lipumba amesema kwa mujibu wa kifungu cha 79(2)(a) cha katiba ya chama hicho kinasema kuwa, Mkutano Mkuu wa Taifa unaweza kuchukua hatua za kinidhamu zozote zile, zikiwamo kumuachisha au kumkufukuza uongozi au uanachama au yote mawili Mwenyekiti wa chama hicho, Hivyo kutokana na kifungu hicho, anavuliwa uanachama na Mkutano Mkuu wa Taifa, sio baraza la uongozi ambalo na lenyewe halijakidhi matakwa ya katiba ya chama, kilichofanyika Zanzibar ni sawa na kikao cha harusi.

Lipumba amesema Katiba ya chama hicho inawataka wajumbe 22 kutoka Kamati Kuu ya chama kudhuria kikao ndipo maamuzi yaweze kufanyika katika kikao hicho, lakini idadi ya wajumbe waliohudhuria kutoka Bara ni 9 ambao kati yao, watatu wajumbe wa kamati kuu na sita ni wanachama wa kawaida.

Amesema katika katiba hiyo kifungu cha 83(5) kinasema, baraza hilo linaweza kuchukua hatua za kinidhamu ikiwa ni pamoja na kutoa onyo kwa maandishi, karipio kali, ambapo kabla ya kufikia uamuzi huo, Katibu Mkuu alipaswa kuitisha Mkutano Mkuu ambao pamoja na mambo mengine, ulitakiwa kumjadili ili wajumbe waweze kumpigia kura ya kumwondoa. Pia alisema alipaswa kupewa nafasi ya kujieleza katika mkutano mkuu ndipo wajumbe waamue hatua ya kumchukulia.

Prof Lipumba amesema kufuatia hayo yeye bado ni mwenyekiti halali na yupo ngangari katika kukijenga chama na hafukuziki, hasusi wala hawezi kukihama chama hicho badala yake amejiwekee mikakati ya kuhakikisha anawaunganisha wanachama wa chama hicho katika kipindi hiki ambacho chama hicho kimetoka kwenye mgogoro wa uongozi uliosababisha Msajili wa vyama vya siasa kuingilia kati.

Amesema wanapaswa kukaa pamoja na kuondoa tofauti zilizopo ili waweze kukijenga chama.

Katika hatua nyingine, Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imesema wanaendelea kumtambua Profesa Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa chama hicho kwani haijapokea mabadiliko yoyote ya uongozi kutoka katika chama hicho. Pia imeeleza kuwa msimamo wao upo pale pale kwamba Lipumba ni Mwenyekiti halali wa CUF kwa mujibu wa Katiba ya chama hicho mpaka hapo itakapoelezwa tofauti kwa kusimamia sheria za vyama vya siasa na Katiba ya chama hicho.

 

Tukumbushane baadhi ya ahadi za JPM kipindi cha uchaguzi
Polisi Kenya waongeza nguvu uchunguzi wa Al-Shabaab