Mwenyekiti wa Chama cha wananchi CUF, Prof Ibrahimu Lipumba ikiwa siku moja baada ya Mahakama kuu ya Tanzania kumtambua kwa nafasi hiyo leo Machi 19, 2019  amezungumza na vyombo vya habari akiwataka wapemba na wanachama wengine wa CUF wanaotaka kukihama chama hicho na kuhamia ACT Wazalendo kutofuata upepo huo.

Amewataka wanachama hao kuchanganya akili zao na kutokurupuka kwa kumfuata Maalim Seif kwa kuhamia ACT-Wazalendo.

Lipumba amesema yeye ni moja ya viongozi waliopigania haki ya wazanzibari chini ya bendera ya CUF.

”Ndugu zangu wapemba chama hiki ni cha kwenu hakuna haja ya kumfuata mtu ambaye ukifuatilia mienendo yake utagundua hakuwa na nia nzuri na chama chetu zaidi ya kutaka Usultani, Chama hiki sio cha mtu ni cha wanachama na wanachama ndio nyie” amesema Lipumba.

Aidha amewataka wanachama wa CUF kutofanya makosa ya jinai pasipo lazima kwani tayari kuna baadhi ya wanachama wameanza kuchoma bendera za CUF na kupaka rangi ya ACT Wazalendo ofisi za CUF.

”Ndugu zangu wanachama  wa Zanzibar msiingie jazba, mkaanza kufanya makosa ya jinai, kuchoma bendera ya Chama ni kosa la jinai, kubadilisha ofisi ya chama ni kosa la jinai”. ameongezea Lipumba.

Aidha, Hamidu Bobali mbunge wa jimbo la Mchinga mkoani Lindi chini ya CUF, amerejea CUF kuunga mkono  juhudi za ujenzi wa Chama cha Wananchi CUF baada ya kipindi cha muda mrefu kuwa katika msuguano mkali baina ya wanachama wa chama hicho.

Hivyo amewaomba wabungena viongozi wengine kurejea nyumbani kukiendeleza chama hiko kwani tayari mahakama imeshatenda haki na kuamua kumtambua Prof Lipumba kama Mwenyekiti wa chama hiko.

 

Tanzania yatoa msaada Msumbiji, Malawi na Zimbabwe
Wafanyabiashara ya viumbe pori wamlilia Magufuli