Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa ameagiza kuvunjwa mkataba na mhandisi mshauri wa kampuni ya DONCONSULT LTD ya jijini Dar es Salaam, anayefanya upembuzi yakinifu wa miradi ya maji ya miji minne ya Kyaka, Bunazi, Muleba, Biharamulo na Ngara Mkoani Kagera kutokana na kutoridhishwa na utendaji kazi wa kampuni hiyo katika miradi mingi anayopewa.

Waziri Mbarawa ametoa agizo hilo jana Julai 12 mwaka huu wakati wa ziara yake Wilayani Missenyi baada ya kupewa taarifa kuwa mhandisi mshauri wa mradi huo kuwa ni Donconsult ltd ambayo imepewa kazi hiyo toka mwezi Aprili mwaka huu inayotakiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu lakini maendeleo yake ni duni.

Amesema kuwa, mhandisi huyo amepata kazi kwa njia za ujanja ujanja kutokana na kuelewana na baadhi ya watumishi wa wizara ya maji wasiokuwa waaminifu ambao wanapewa fedha kumsaidia kupata kazi ingali, uwezo wake wa kutekeleza miradi hiyo ni mdogo jambo linalopelekea kukwama kwa miradi.

”Mhandisi huyo hatufai hata kidogo, kashatupiga pesa nyingi na miradi yote anayoitekeleza hakuna mradi hata mmoja ambao unafanya kazi kwa ufanisi, futeni mkataba huo na badala yake kazi hiyo itafanywa na mamlakaza Maji za MUWASA NA BUWASA, na nimeshasema kampuni hiyo hakuna kupata kazi katika wizara yangu.” alisema Waziri Mbarawa.

Aidha, Waziri Mbarawa amesema kuwa miongoni mwa miradi ambayo imesanifiwa na mhandisi mshauri ni pamoja na mradi wa maji wa Handeni –Tanga na mwingine ukiwa mkoani Iringa ambayo mpaka sasa Serikali imelipa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji lakini miradi hiyo imekwama kutokana na usanifu kuwa na kasoro.

Hata hivyo, Prof. Mbarawa akiwa wilayani Karagwe alitembelea mradi wa maji wa Kata ya Nyakabanga ambapo alikagua uendeshaji wa mradi huo uliojengwa katika kijiji cha Chabuhola na kumuagiza Mhandisi wa Maji mkoa siku ya Jumatatu kwenda kukagua mabomba yaliyotumika kwenye Mradi huo baada ya wananchi kulalamikia kutopata maji kutokana na mabomba kupasuka.

Video: Rais Museveni kujenga vyumba vya madarasa Nyabirezi wilayani Chato
LIVE CHATO: Rais Magufuli akiagana na rais wa Uganda, Yoweri Museveni