Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa amezindua rasmi Kampeni ya Upandaji Miti kandokando ya vyanzo vya maji nchi nzima mkoani Mtwara kwa lengo la kuhakikisha vyanzo hivyo vinatunzwa na kuwa endelevu kwa miaka mingi ijayo.

Amezindua kampeni hiyo kwa kupanda miti nane katika chanzo cha Maji Mtawanya kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara Mjini na kuzitaka Bodi zote za Mabonde tisa nchini kuweka mkazo na mipango madhubuti ya kusimamia na kutunza rasilimali za maji ziweze kuwa endelevu.

Ametoa agizo hilo kutokana na uvamizi na uharibifu mkubwa wa vyanzo vya maji katika maeneo mengi kwa sasa nchini, hali inayohatarisha kiasi kikubwa cha maji kupungua kutokana na vyanzo vingi kukauka.

Ametoa tamko hilo kwa kuzingatia Sheria ya Maji Na, 11 ya Mwaka 2009 inayokataza kufanya shughuli za kibinadamu katika vyanzo vya maji, na ikieleza kuwa shughuli zote za kibinadamu zifanyike umbali wa mita 6o kutoka chanzo cha maji kilipo.

‘‘Hatutaki kupata hasara kwenye miradi tunayowekeza fedha nyingi, halafu baadae iwe kama magofu kwa kukosa maji. imefika hatua kuwa ni lazima tuchukue hatua za lazima kulinusuru taifa letu na uhaba wa maji. Niwatake wananchi watoe ushirikiano wa karibu na Serikali kuhakikisha vyanzo vyetu vyote vinakuwa endelevu kwa kuzalisha maji ya kutosha,” amesema Prof. Mbarawa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mjini, Evod Mmanda amesema kuwa ni muhimu zoezi la upandaji miti liwe endelevu lenye kuzingatia upandaji wa miti na kuachana na miti isiyo rafiki na maji kwa lengo la utunzaji wa maeneo yote yenye vyanzo.

Hata hivyo, Serikali kupitia Wizara ya Maji hivi karbuni imetoa Shilingi Bilioni 2.3 kwa ajili ya malipo ya madai kwa wakandarasi mbalimbali wanaotekeleza miradi ya maji katika Mkoa wa Mtwara, ambapo uzalishaji wa maji kwa siku kwa mji wa Mtwara umefikia lita milioni 10, huku mahitaji kwa siku ni lita milioni 13.7.

 

Masauni awatahadharisha wamiliki wa shule
Chadema yawakaanga Kubenea na mwenzie