Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Serikali itawalipa fidia wananchi waliopisha ujenzi wa barabara nchi nzima kisheria hivyo waondoe wasiwasi.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Mwigumbi Mkoani Shinyanga alipokuwa akikagua ujenzi wa barabara ya Mwigumbi – Maswa yenye urefu wa Km 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami na mkandarasi wa Kampuni ya CHICO na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake ambao unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 61.

“Kila anayestahili kulipwa fidia atalipwa kama sheria inavyoelekeza na endapo akatokea yeyote mwenye malalamiko Serikali ipo itamsikiliza, hivyo wananchi ondoeni hofu yeyote kwani Serikali ipo kwaajili yenu”, amesema Prof. Mbarawa.

Aidha, Prof. Mbarawa amewahimiza makandarasi wote nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa maeneo husika inapopita miradi ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali ili kuwapatia kipato na kuinua uchumi wao.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Shinyanga Eng. Batholomeo Ndirimbi amesema kuwa mpaka sasa tayari fedha zimetengwa kwa ajili ya ulipaji fidia na watahakikisha kuwa fedha hizo zinalipwa kwa watu sahihi wanaostahili fidia hizo.

 

Saudi Arabia yamchunguza mwanamke aliyeposti picha za utupu mtandaoni
Kubenea amshukia Ndugai, asema kiatu alichovaa hakimtoshi