Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome, amesema Taasisi za Haki za Binadamu za nchi za Afrika Mashariki zinawajibu wa kutoa elimu kuhusu Haki za Binadamu kwa umma na kuongeza kuwa haki za binadamu ndio chachu ya maendeleo katika nchi yeyote.

Ameyasema hayo leo Novemba  8, 2016,  jijini Dar es salaam alipokuwa akifungua  mkutano mkuu wa mwaka wa taasisi zinazosimamia Haki za Binadamu katika nchi za Afrika Mashariki na kuzitaka kutoa elimu ya kutosha kwa umma.

Prof. Mchome amesema jukumu la ulinzi na usimamizi wa haki za binadamu katika eneo la Jumuiya hiyo ni la kila nchi mwanachama, kwa kuwa msingi wa maendeleo wa nchi yoyote duniani hupatikana katika sehemu yenye hali ya utulivu na maeleweno.

Aidha, Prof. Mchome amesema kuanzia mwezi Mei hadi Septemba mwaka huu, nchi zote za Afirika Mashariki ziliwasilisha taarifa zao kuhusu hali ya haki ya kibinadamu katika mataifa yao, mjini Gevena Uswisi, ambapo ripoti hizo zitatumika katika kujadili changamoto zilizojitokeza na hatua za kuchuliwa katika kuboresha.

Ameongeza kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizopiga hatua kubwa katika kuimarisha haki za kibinadamu duniani ingawa yapo maeneo kadhaa yenye migogoro  ikiwemo migogoro ya wakulima na wafugaji, ingawa Serikali imechukua hatua za makusudi  za kukabiliana na hali hiyo.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAG), Mary Massay amesema suala la haki za binadamu ni dhana mtambuka kwa kuwa inagusa sekta muhimu za maisha ya binadamu ikiwemo elimu, maji, ardhi, maliasili na kadhalika.

Video: Wabunge wakubali msimamo wa Serikali
Video: Mfumuko wa bei wazidi kushuka nchini