WAZIRI  wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amekabidhi nyaraka za ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 20 wa kitanzania wanaokwenda kusoma fani za mafuta na gesi katika ngazi za uzamili na uzamivu nchini China.

Watanzania hao 20 wamepatikana kutokana na mchujo na Wizara hiyo ukihusisha watanzania 89 kwenye ngazi mbalimbali za elimu nchini.

Akizungumza wakati wa kukabidhi nyaraka hizo leo Jijini Dar es Salaam, Prof. Muhongo alisema kuwa wizara ya Nishati na Madini imekuwa ikisomesha vijana wa kitanzania nje ya nchi kwa ajili ya kusomea masuala ya mafuta na gesi.

“Serikali ya China imetoa nafasi kwa vijana wa kitanzania kusoma nchini mwao na kwa jinsi ilivyo tukaona ni vyema tuzitangaze nafasi hizi kwa Watanzania wote kupitia wizara yetu ili waweze kuisaidia nchi yao na baada ya mchujo leo hii tunawakabidhi nyaraka zao za masomo” alisema Profesa Muhongo

Aidha Profesa Muhongo aliwataka vijana hao kuitumia vyema nafasi waliyoipata na kuhakikisha wanasoma kwa bidii kwani nchi inahitaji wataalamu wa kutosha katika sekta ya mafuta na gesi ambayo inakua kwa kasi ya haraka nchini.

Kwa upande wake Naibu Balozi wa China Nchini Bw.Gou Haodong amewaasa watanzania hao kusoma kwa bidii wakiwa nchini china na kuhakikisha wanafikia malengo yao ya kitaaluma.

Pia amewaasa kuhakikisha wanawafundisha watu wa china utamaduni wa mtanzania na wawe mabalozi wazuri wa nchi yao.

Serikali ya China inatoa ufadhili wa nafasi 20 kwa mwaka kwa kipindi cha miaka mitano kwa watanzania ili kujifunza masuala ya Gesi na Mafuta nchini mwao kupitia Wizara ya nishati na madini.

Vijana Watakiwa Kujenga Tabia Ya Kujifunza Ili Kuibua Mawazo Endelevu
Uchaguzi Wa Urais Waanza Gabon