Serikali imewataka wakuu wa shule za Msingi na Sekondari nchini pamoja na Bodi zake kuhakikisha wanachukua hatua stahiki dhidi ya vitendo vya utovu wa nidhamu unaofanywa na baadhi ya wanafunzi shuleni.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako jijini Dar es salaam,wakati wa mdahalo kuhusu kujenga na kukuza Maadili, Haki za binadamu, Uwajibikaji, Utawala bora na Mapambano dhidi ya rushwa uliolenga kukuza na kusimamia maadili kwa vijana.

Aidha, Prof. Ndalichako aliziagiza bodi hizo kusimamia sheria, kanuni na taratibu kuhusu maelekezo mbalimbali yanayotolewa na kuachana na siasa katika suala zima la maadili kwa wanafunzi.

“Suala la kukuza na kusimamia maadili siyo jukumu la Rais pekee, au jukumu la taasisi pekee, bali ni jukumu la jamii nzima, hivyo tunatakiwa sote kushirikiana kwa pamoja katika ngazi zote”, alisema Prof. Ndalichako.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa, (TAKUKURU) Valentino Mlolowa alisema kuwa mdahalo huo una lengo la kuwawezesha wanafunzi kupata elimu kuhusu Maadili, Haki za Binadamu, Uwajibikaji, Utawala bora na Mapambano dhidi ya Rushwa kwa kuamini wanafunzi ni kundi lenye nguvu katika kuleta mabadiliko katika jamii.

Serikali kuhifadhi kumbukumbu za urithi usioshikika
NACTE kuvifungia vyuo vikuu 26