Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule maarufu kama Profesa Jay, ametoa maoni yake kuhusu ushauri wa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe aliyewataka wasanii wa Tanzania kuacha kuimba nyimbo zenye jumbe za kisiasa kwani hawatafanikiwa.

Profesa Jay ambaye ni rapa nguli wa kizazi kipya aliyewahi kuweka rekodi maalum ya albam yake ya ‘Mapinduzi Halisi’ iliyokuwa na jumbe zenye mlengo wa kisiasa na kijamii, amesema ameshangazwa na kauli ya Waziri.

“Kuwaambia wasanii kuwa waimbe nyimbo za maisha yao tu na washindwe kuimba vitu vingine, maana yake unataka kutoa ‘green light’ kwa wasanii sasa waanze kuimba mambo ya mapenzi… nakupenda, nakupenda..,” alisema Profesa Jay.

“Maana yake unaweza kuchochea kuhusu masuala ya mapenzi tu na kushindwa kufanya vitu vya kijamii ambavyo vingeweza kulipeleka taifa letu mbele. Mimi naamini msanii ana sauti kubwa na anaweza kupaza sauti positively na ikasaidia taifa letu ideologically (kiitikadi), socially (kijamii), culturally (kitamaduni), economically (kiuchumi), politically (kisiasa) pamoja na sustainable development (maendeleo endelevu),” aliongeza.

Mbunge huyo alidai kuwa wapo wasanii walioimba kuhusu siasa na masuala ya kijamii kama 2Pac, BIG, Bob Marley, Lucky Dube na wengine ambao walisaidia dunia kuhama katika ngazi moja kijamii hadi ngazi nyingine.

Hata hivyo, Profesa Jay alikubaliana na hoja ya Waziri Mwakyembe kuwa wasanii hawapaswi kuitukana Serikali, akieleza kuwa wanapaswa kuachwa watoe mawazo yao mbadala ikiwa ni pamoja na kuisifia Serikali.

Akizungumza Bungeni mjini Dodoma, Waziri Mwakyembe aliwashauri wasanii kuachana na nyimbo za siasa kwani hawatafanikiwa kwakuwa hakuna msanii ambaye alijikita katika kuimba siasa na akafanikiwa. Alitoa mifano ya wasanii kama Diamond, Ali Kiba, Chameleone na wengine. Dk. Mwakyembe alisisitiza kuwa kazi ya wasanii ni kuburudisha.

Gidabudai: Tupo Tayari Kwa Michuano Ya Afrika Mashariki Na Kati
Stand Utd Watamba Kuzima Ndoto Za Ubingwa Msimbazi