Msanii mahiri na gwiji wa muziki wa bongo fleva, Joseph Haule maarufu Profesa Jay amefunguka mtazamo wake juu ya mwenendo mzima wa tasnia ya muziki huo kwa sasa, ukilinganisha na namna ambavyo wasanii wa zamani walivyokuwa wakifanya.

Jay amesema anachokiona ni kuwa wasanii wengi wa sasa ni wavivu katika kufikiria na kuzalisha aina ya maudhui yenye tija kwa hadhira, jambo linalopelekea wengi wao kuishia kutengeneza nyimbo zilizo chini ya ubora na viwango vyenye kustahiki kwa hadhira na zenye kuishi kwa muda mfupi tofauti na walivyokuwa wakifanya wasanii wa zamani ambao mpaka sasa nyimbo zao zinaishi.

”Watu wanataka wepesi tu, dunia imekuwa kama kijiji, kiswahili kinapasua anga lakini pia muziki wetu kwa kiasi chake  tumeanza kupasua kwenda mataifa mengine, laikini badala ya watu kufanya kitu kilichokuwa sahihi sasa hivi, watu wanataka wepesi, hawataki kuhangaika kuhusu kuandika mashahiri na kuweka ubunifu kwenye kazi zao,” alisema Profesa jay.

Pamoja na hayo profesa amegusia swala la baadhi ya wasanii wenye kasumba ya kufuata mkumbo na kujikuta wanajihusisha na kila aina ya muziki unaokuwa unatamba kwa wakati huo bila kujali kudumisha na kuenzi utamaduni wa muziki wa bongo fleva ili kuipeperusha bendera ya Tanzania kwa muziki wa ndani na si wa kutoka mataifa mengine.

”wasanii wengi wasasa kila mmoja anataka kuimba Amapiano, kwa sababu ni mziki usioumiza kichwa, mwepesi sana, sasa ule ni uvivu wa kuandika na content wakati nchi yetu tuna mambo mengi ya kuzungumzia, unaweza hata ukaongelea mapenzi lakini tuongelee mapenzi katika namna ambayo hata wazee wetu walikuwa wakifanya kwenye nyimbo zao, sasa hivi tumekuwa wavivu yani tunataka hela bila kufanya kazi” aliongeza.

Katika kuendelea kubainisha ukweli kuhusu anachokiona, Profesa ameweka wazi namna jitihada za kufanya muziki wenye vigezo vinavyostahili ulivyo changia kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya kifikra kwa wazazi pamoja na taasisi mbali mbali kuanza kuitazama tasnia ya muziki kwa jicho la tatu, kiasi cha baadhi ya wazazi waliokuwa wakihisi muziki ni uhuni, kuanza kuwaruhusu watoto wao kwa kuwapa uhuru wa kujihusisha na muziki kwa imani ya kuwa ni sawa na kazi nyingine yeyote.

Profesa Jay amesema kitendo cha wasanii kujikita katika kuandika nyimbo zisizokuwa na maadili, kinaashiria kuwa wazazi walioamini muziki ni sehemu sahihi ya kujiajiri waanze kuwakataza watoto wao kujihusisha na sanaa hiyo.

”Kwasasa naona watu wamefikia mwisho wa kufikiri na hawataki tena kizazi kingine kije kuimba tena, kwa sababu vitu vinavyoimbwa sasa hivi vinapelekea watu wanashindwa kusikiliza muziki na wazazi wao, maana yake ni kwamba wazazi wafunge tena mlango watoto wao wasije kuimba tena muziki kwa sababu content zimeshapotea.”

Profesa Jay ameyasema hayo kupitia mahojiano maalumu aliyofanya na eatv, ambapo alihitimisha kwa kutoa rai kwa wasanii kuwekeza kama wasanii wa zamani walivyowekeza, kupitia mafanikio ambayo wamekuwa wakiyapata, wajitahidi kutengeneza maudhui yenye tija na wasisahau kukibeba kiswahili pia japo si vibaya kuweka vionjo vya lugha za kigeni.

Serikali yazindua mkakati wa kitaifa wa magonjwa yasiyoambukiza.
Mkuu wa magereza afutwa kazi baada ya wafungwa 3 kutoroka - Kenya