Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amekutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa Norway kwa nchi zinazoendelea (Norwegian Investment Fund for Developing Countries – Norfund), Tellef Thorleifsson.

Mazungumzo hayo yamefanyika jana katika ofisi ndogo za wizara jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine, Prof. Kabudi pamoja na Bw. Thorleifsson wamejadili masuala yanayohusu fursa za uwekezaji na biashara kati ya Tanzania na Norway.

“Kwa kweli sisi tunafurahishwa na mradi wa Africado ambao umewekezwa katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro kwani umekuwa ukizalisha maparachichi yanayopelekwa nchi mbalimbali za Ulaya kama vile Uholanzi, Uingereza, Ufaransa, Hispania, Ureno, na Mashariki ya Kati, na kuisaidia serikali kukuza pato lake la taifa,” Amesema Prof. Kabudi na kuongeza kuwa mradi huo umetoa fursa za ajira takribani 600 kwa wananchi wa Tanzania.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Uwekezaji wa Norfund, Thorleifsson amesema kuwa lengo la mkfuko huo ni kuwekeza katika miradi mbalimbali ndani ya nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ili kuzisaidia nchi hizo kukuza uchumi wake.

“Lengo letu ni kuwekeza katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambapo hadi kufika mwishoni mwa 2018 tayari mfuko ulikuwa umewekeza nchini Tanzania kiasi cha Dola za Marekani milioni 160 katika miradi mbalimbali katika sekta za nishati, fedha, chakula na kilimo. Uwekezaji huo umeifanya Tanzania kuwa nchi ya nne katika nchi zinazonufaika na miradi ya Norfund,” amesema Bw. Thorleifsson

Norfund ni taasisi iliyo chini ya Serikali ya Norway yenye jukumu la kuwekeza mitaji na utaalamu katika uanzishwaji wa miradi mbalimbali endelevu kwenye nchi zinazoendelea kwa lengo la kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Ziara imetoa fursa kwa pande zote mbili kuweza kujadili namna bora ya kuboresha maeneo ya vipaumbele katika sekta ya uwekezaji.

Mke wa Bryant avunja ukimya kifo cha mumewe na mtoto
Chadema wamzungumzia mgombea Urais wao 2020