Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaama, Profesa Kitila Mkumbo ameukosoa mdahalo uliandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), uliorushwa moja kwa moja na kituo cha runinga Star TV, wikendi iliyopita, akidai kuwa ulilenga kuipigia debe CCM.

Profesa Kitila amekosoa muundo wa Mdahalo huo uliolenga katika kujadili namna ya kulinda amani, umoja na haki katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu, kwa kutokuwa na pande zinazokinzana kimtazamo hivyo kukosa sifa ya kuwa mdahalo bali mazungumzo ya kuipigia debe CCM.

Kadhalika, ametilia shaka mabadiliko ya mazingira mdahalo huo ukilinganisha na midahalo iliyoandaliwa awali na Taasisi hiyo, ikiwa ni pamoja mabadiliko ya kituo cha runinga, watoa mada kuwa wote wa mlengo mmoja wa CCM huku wakimuondoa Profesa Baregu ambaye ni mshauri wa Chadema.

Mhadhiri huyo mwandamizi aliwakosoa watoa mada walioandaliwa ambao ni Joseph Butiku, Balozi Getrude Mongela na Hamphrey Polepole. Alisema kuwa watoa mada wote walifanya mazungumzo ya kuitetea CCM, chama ambacho alidai wamekuwa wakikikosoa kwa kipindi chote cha miaka 10.

Hii ni sehemu ya alichoandika Profesa Kitila kwenye Facebook.

“Nimefuatilia kwa kiasi ‘mazungumzo’ ya ndugu Butiku, Mama Mongela na ndugu Polepole. Nayaita Mazungumzo na sio mdahalo kwa sababu hapakuwa na hoja kinzani. Wamekutana watu ambao wanakubaliana na kushabihiana kifikra na kimlengo. Kwa kweli wametumia vizuri fursa hiyo kupigia debe CCM. Sio mbaya, wana haki.

“Hata hivyo, ninaangalizo. Kwa takribani miaka 10 tangu JK (Rais Jakaya Kikwete) aingie madarakani, Mwalimu Nyerere Foundation wamekuwa vinara wa kuinanga CCM na kutoonesha jinsi chama hiki kilivyobadilika na kuwa cha hovyo.

“Naamini mlimaanisha na wala hamkuwa na chuki binafsi na JK. Sasa itakuwa vizuri mkatueleza Watanzania wenzenu ni lini hasa chama hiki kiliacha yale mabaya mliyotueleza katika miaka 10 iliyopita?”

Sentensi 3 Zinazotajwa Kawaida, Ambazo Mwanamke Hapaswi Kabisa Kumwambia Mmewe/Mchumba
Kingunge Atumia Maneno Makali Kumjibu Dkt. Bana