Matokeo ya uchaguzi wa Urais wa Marekani uliompa ushindi wa kura za wajumbe mgombea wa Republican, Donald Trump huenda yakabadilika, japo ni nadra.

Akizungumza katika mahojiano maalum na mtangazaji wa 100.5 Times Fm, Erick Martin moja kwa moja kutoka Washington DC, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Maryland, Profesa Nicholas Boaz amesema kuwa endapo mchakato wa kurudia kuhesabu kura katika majimbo matatu yaliyompa ushindi Trump ukikamilika na kuonekana kuwa na dosari zilizotajwa, huenda yakapelekea  mwanasiasa huyo kupokonywa urais.

“Kama kuna ukweli huo wa kuona kwamba labda Clinton alikuwa ameshinda katika majimbo yale [matatu], inawezekana kabisa. Matokeo yanabadilika na itabidi mahakama iamue sasa,” alisema Profesa Boaz.

“Kama ni kura hizo zinazohesabiwa ndizo zinamfanya ashinde, kura hizohizo zinaweza kumfanya akashindwa na akanyang’anywa urais huyo Trump,” aliongeza.

Hivi karibuni, mwanasiasa ambaye pia ni mwanaharakati wa nchini humo, Dkt. Ellen Stein alianzisha harakati akitaka kura zirudiwe kuhesabiwa katika majimbo ya Wisconsin, Michigan na Pennsylvania ambapo alidai kuna kasoro nyingi za kitakwimu. Katika majimbo hayo, Trump alipata ushindi mwembamba.

Kambi ya Clinton imetangaza kuunga mkono zoezi la kuanza kuhesabu upya kura za majimbo hayo lililoanza, baada ya Serikali ya nchi hiyo kueleza kuwa kuna uwezekano mkubwa wa wadukuzi wa urusi kuingilia uchaguzi katika majimbo hayo.

Urusi imekanusha vikali tuhuma hizo dhidi yake na kueleza kuwa haikujihusisha kwa namna yoyote na uchaguzi wa Marekani.

Ali Kiba amkejeli Diamond kuhusu ‘Pete ya Kijani’
Lipumba: Maalim Seif Waganga watakudanganya sana…