Waziri wa ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi amesema kuwa halmashauri zina wajibu wa kuyasimamia mabaraza ya ardhi ya Kata katika maeneo mablimbali nchini.

Ameyasema hayo jijini Dar es salaam wakati akizungumza na wananchi wa wilaya ya Kinondoni wakati wa mkutano wa kusikiliza migogoro ya ardhi kupitia Programu ya ‘Funguka’, ambapo amesema kuwa halmashauri kupitia kwa mwanasheria wake zinapaswa kujua maamuzi yote yanayotolewa katika Mabaraza ya Ardhi ya Kata.

Amesema kuwa, pamoja na kilio cha wananchi wengi dhidi ya Mabaraza ya Ardhi ya Kata katika maeneo mbalimbali lakini upo utaratibu mzuri uliopangwa kuhusiana na Mabaraza hayo ingawa yameachwa yajiendeshe yenyewe huku Halmashauri chini ya Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ikiyaangalia bila kufuatiliwa.

”Uonevu wowote unaofanyika katika mabaraza ya ardhi ya kata basi mwanasheria wa halmashauri anapaswa kulaumiwa kwa kuwa ana uwezo wa kuwaita waliotoa maamuzi na kuwahoji dhidi ya uonevu uliofanyika sambamba na kuhakikisha maamuzi yanayofanyika katika mabaraza hayo yanazingatia haki.’’Amesema Lukuvi

Aidha, Lukuvi ameelezea pia utaratibu wa kupiga mnada nyumba za watu walioshindwa kulipa madeni mara baada ya kukopa fedha na hati ya nyumba kuwekewa dhamana bila kufuata utaratibu lengo likiwa ni kutwaa nyumba za wahusika.

Akizungumzia suala hilo kufuatia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kuelezea uonevu wanaofanyiwa baadhi ya wananchi wake pale wanapokopa fedha kwa makubaliano hati ya nyumba kuwekwa dhamana, amesema kuwa muda wa kurudisha fedha unapofika mhusika huzima simu kwa siku kadhaa na baadaye kwenda Baraza la Ardhi la Kata kudai kupewa nyumba kwa maelezo kuwa mkopaji alishindwa kulipa.

 

Naibu waziri Mgumba asisitiza ushirikiano na Ueledi kazini
Ujumbe wa Dogo Janja waibua maswali