Wadau wa muziki wa hip hop wiki hii wameamshwa na ngoma ya makombora ya mistari kutoka kwa rapa Pusha T kwenda kwa Drake, akijibu mapigo yaliyotoka kwa rapa huyo wa Young Money.

Pusha T ameonekana kumvuruga Drake kupitia ngoma aliyoiachia kwa mfumo wa mitindo huru aliyoibatiza jina la ‘The Story of Adidon’, akijibu mashambulizi ya ‘Duppy Freestyle’ ya Drake iliyolenga kumnyoosha.

Kupitia ‘The Story of Adidon’, Pusha T amemlazimisha Drake kutoa maelezo kuhusu mtoto wa kiume aliyezaa na mchezaji  wa filamu ya ngono na kuiweka siri kwa muda mrefu.

Aidha, picha ya Drake akiwa amevalia kinyago cheusi usoni ambayo ilithibitishwa kuwa ni halisi iliyotumiwa na Pusha T kama jarada la ngoma hiyo, imemlazimu kutoa maelezo mengine ya ziada.

Drake ametumia mtandao wa Instagram kueleza kuwa ni kweli ana mtoto aliyezaa na mchezaji huyo wa filamu za ngono na kwamba amekuwa akitoa fedha za matumizi kama baba tangu alipozaliwa.

Watu wa karibu wa rapa huyo wanadai kuwa alipanga kumuweka wazi mtoto huyo kwenye albam yake ijayo. Hata hivyo, inaonekana amechelewa kufichua hadi amefichuliwa.

Rapa huyo pia amelazimika kujieleza kuwa kuvaa sura nyeusi hakukuwa na lengo baya la ubaguzi wa rangi, bali ni picha iliyotoka kwenye mradi wa filamu aliyoigiza mwaka 2007 ingawa haikutoka.

Drake amedai kuwa katika filamu hiyo, aliigiza kama kijana mweusi anayenyanyaswa kwenye kiwanda cha muziki na burudani lakini ana kipaji kikubwa.

Aidha, Pusha T ambaye hivi sasa anaendelea kuuza albam yake mpya ya Daytona, amekosolewa vikali kwa kuvuka mstari wa ustaarabu na kuwavaa baba na mama yake Drake kwenye ngoma hiyo. Rapa huyo amekiri kufanya kosa na kudai kuwa hakudhani kama ingechukuliwa hivyo.


‘The Story of Adidon’ imekuwa gumzo na kuzungumziwa na watu maarufu ikiwa ni pamoja na 50 Cent, Ja-Rule, Ice Cube, TI, Jamie Foxx na wengine.

Pia, ngoma hiyo imeamsha upya bifu kati ya 50 Cent na Ja Rule ambao wameanza kushambuliana kwenye mitandao ya kijamii.

Kinachosubiriwa hivi sasa ni jibu la Drake ambaye wengi wanaamini hajakaukiwa mistari. Inaonekana kama Drake alishinda kirahisi dhidi ya Meek Mill lakini kwa Pusha T amekutana na kisiki.

Cristiano amuaga Zidane kwa hisia
Tanzia: Mama mzazi wa Mbunge Bashe ameaga dunia mapema leo