Rais wa Urusi, Vladimir Putin ameahidi kuzifuatilia kwa karibu hatua za Marekani zilizotangazwa na Rais Donald Trump kuhusu mpango wa kujenga upya vinu vya silaha zake za kinyuklia.

Putin amezungumzia hatua hizo za Marekani baada ya Trump kutishia kuachana na mpango wa makubaliano ya udhibiti wa makombora yenye uwezo wa kupiga maeneo nyeti ya Ulaya, uliosainiwa mwaka 1987 kati ya viongozi wa dola ya Kisoviet na Marekani, maarufu kama ‘INF treaty’.

Rais huyo wa Urusi ameonya nchi za bara la Ulaya kuwa zitakuwa kwenye hatari ya mstari wa mapambano kama Marekani na Urusi zitafutilia mbali makubaliano hayo ya mwaka 1987.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita alipoalikwa kama mgeni rasmi kwenye mjadala wa Valdai, Putin alisisitiza kuwa Urusi haimuogopi mtu yeyote wala nchi yeyote.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa nchi yake haitaanzisha mashambulizi kwa nchi yeyote lakini ikipigwa itajibu kwa kipigo kikali zaidi. “Tupige, tukupige,” anakaririwa.

Akifafanua kauli yake, aliweka ucheshi kuwa muathirika wa kipigo hicho cha majibu hatakuwa na muda wa kutubu kwani kipigo kitampeleka moja kwa moja mbinguni.

Mwaka jana, Trump amewahi kukaririwa akionya kuwa hakuna atakayesalimika katika vita ya makombora ya nyuklia kati ya nchi yake na Marekani.

“Sidhani kama kuna atakayesalimika kwenye mgogoro huo wa kinyuklia,” alisema Putin. “Lakini kuna matumaini ya utulivu kwetu wakati wote, hadi itakapofikia hatua ya kutusukuma na kuwa tayari kutuzika,” aliongeza.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya kivita wamekaririwa na BBC kuwa mgogoro huo utabaki kuwa katika kauli za viongozi na hautakuwa na madhara ya hatua za kweli za kijeshi, kwani kauli hizo na uhusiano wa nchi hasimu pamoja na washirika wao haujafikia hata robo ya joto la vita baridi.

Imeripotiwa kuwa Putin na Trump wanaweza kukutana hivi karibuni jijini Paris nchini Ufaransa kuzungumzia joto la mkataba wa INF.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Oktoba 26, 2018
Video: Majaliwa apokea ripoti ya uchunguzi wa  ajali ya kivuko cha MV Nyerere