Idara za upelelezi wa makosa ya jinai za Illinois na Georgia nchini Marekani, vimeeleza kuwa kuna taarifa za kiintelijensia zinazomhusu R Kelly kupanga njama za kukimbilia barani Afrika, kukwepa mashtaka ya unyanyasaji wa kingono kwa wasichana wadogo yanayoandaliwa dhidi yake.

R Kelly amekuwa mada kuu ndani ya kipindi cha wiki hizi mbili tangu makala maalum inayowaonesha wanawake kadhaa wanaodaiwa kunyanyaswa kingono na mwimbaji huyo walipokuwa na umri wa kati ya miaka 14 hadi 16 na mwingine miaka 19, kuachiwa rasmi kwa ajili ya umma.

Makala hiyo ya video iliyopewa jina la ‘Surviving R Kelly’, imewasha moto na kuwaibua watu wengi zaidi, huku lebo ya muziki aliyokuwa akiifanyia kazi ikimtema rasmi na nyimbo zake zote kuondolewa kwenye mitandao ya kuuza muziki.

Waathirika wa sakata hilo la R Kelly wanadai kuwa mwimbaji huyo alikuwa na magonjwa ya zinaa yasiyotibika na kwamba alikuwa anayasambaza kwa watoto wa kike kwa makusudi.

Lady Gaga alikuwa msanii wa mwisho hivi karibuni kufuata nyayo za wasanii wengine kwa kutangaza kuufuta wimbo aliomshirikisha R Kelly mwaka 2013 ‘Do What You Want [With My Body]’. Wimbo huo tayari umeshaondolewa YouTube na kwenye mitandao mingine.

Hata hivyo, Idara za uchunguzi wa makosa ya jinai zimewataka wanawake wanaomtuhumu R Kelly kujitolea kushiriki katika uchunguzi huo hadi kusimama mahakamani ili kufanikisha nia ya awali ya kumfungulia mashtaka rasmi, vinginevyo ataweza kuondoka nchini humo.

“Hakuna kitu ambacho kinaweza kufanyika kuchunguza tuhuma hizi bila kupata ushirikiano wa kutosha kutoka kwa waathirika wa tukio hili pamoja na mashahidi. Hatuwezi kutafuta haki bila ninyi,” alisema Kim Foxx ambaye ni mwanasheria wa Serikali wa jiji la Chicago.

“Tunahitaji mashahidi halisi na waathirika ambao wanaweza kueleza kinagaubaga simulizi la manyanyaso ya kingono,” aliongeza.

Katika Makala hiyo mpya, imeelezwa kuwa R Kelly mwenyewe ni muathirika aliyewahi kunyanyaswa kingono akiwa na umri wa miaka 13, lakini baada ya kuwa maarufu aligeuka kuwa mnyanyasaji kwa wasichana wadogo akiwemo marehemu Aaliyah.

R Kelly mwenye umri wa miaka 56, alipaswa kusherehekea siku yake ya kuzaliwa Jumanne wiki hii, lakini iligeuka kuwa siku mbaya kwake kwani dunia ya muziki na jamii viliitumia kumsiliba kwa tuhuma hizo.

Haijafahamika endapo atafanikiwa kutimkia barani Afrika anapanga kuelekea nchi gani kwani amewahi kuzuru Afrika mara kadhaa na kufanya miradi mbalimbali ya muziki.

Mwaka 2010 alikuwa nchini Afrika Kusini ambapo aliimba wimbo wake ‘Sign of Victory’ kwenye Fainali za Kombe la Dunia. Pia aliongoza mradi wa One 8 uliowahusisha wasanii wengi wakubwa Afrika. Aliitembelea pia Ethiopia ambapo alifanya matamasha kadhaa makubwa.

Bastola bandia yawaponza wanne watiwa mbaroni
Kanisa Katoliki lapinga matokeo ya uchaguzi DRC