Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC, Pablo Franco Martin amesema amewafuatilia wapinzani wao kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ‘CAF’ Red Arrows ya Zambia, na amebaini Ubora na Mapungufu yao.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo wa Mkondo wa kwanza utaopigwa Jumapili (Novemba 28), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kabla ya kwenda Zambia kucheza mchezo wa Mkondo wa pili utakaochezwa Desemba 05.

Kocha Pablo amesema baada ya kuona Ubora na Mapungufu ya wapinzani wao Reds Arrows, amejipanga kukiimarisha zaidi kikosi chake ili kupata matokeo mazuri katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kumaliza kazi watakapokwenda ugenini.

Pablo amesema anawaamini wachezaji wake wana uwezo wa kupambana na kumpa matokeo chanya katika mchezo huo ya kimataifa pamoja na Ligi Kuu Tanzania Bara ambayo inaendelea.

Amesema kwa muda ambao amekaa na wachezaji wake, amebaini wana mwelekeo mzuri na wameshaanza kucheza kwa kufuata falsafa yake ya umiliki wa mpira na kucheza soka la ‘pasi nyingi’.

“Tumepata nafasi ya kuwaangalia wapinzani wetu na kujua ubora na mapungufu yao, vyote tunavifanyia kazi, tunajua mchezo utakuwa wa ushindani mkubwa kwa kila mmoja wetu, tunapambana kusaka ushindi, kwa upande wetu tunahitaji kushinda nyumbani,” amesema Pablo.

Ameongeza mchezo huo utakuwa mgumu na wanapaswa kucheza kwa kujitolea asilimia 100 katika muda wote wa dakika 90 ili kufikia malengo na si vinginevyo.

Naye Nahodha na Mshambuliaji wa kikosi cha Simba SC , John Bocco, amewataka mashabiki wa timu hiyo kuendelea kuwapa ushirikiano na kujitokeza kwa wingi kuwashangilia katika mchezo huo wa Jumapili (Novemba 28).

Rais Samia: Hali ya maisha ya Watanzania inazidi kuimarika
Sakata la Chama lafikia patamu