Kamati ya kuzuia na kupambana na dawa zisizoruhusiwa michezoni ya Kanda ya Tano Africa (RADO) imetoa hukumu ya kumfungia mchezaji Mohamed Issa “Banka” kwa kipindi cha miezi 14 kuanzia Disemba 9,2017 na adhabu kumalizika Februari 8, 2019 kutokana na matumizi ya dawa zisizoruhusiwa michezoni aina ya Bangi.

Banka aliyesajiliwa Young Africans Julai mwaka huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro, alikutwa na hatia ya kutumia dawa zilizopigwa marufuku michezoni, aina ya Bangi Desemba 9 mwaka jana baada ya kufanyiwa vipimo wakati wa michuano ya CECAFA Challenge nchini Kenya.

Katika michuano hiyo, Banka aliisaidia Zanzibar kufika fainali baada ya kufunga bao la ushindi kwa penati dakika ya 58 Heroes wakiilaza Uganda 2-1 Desemba 15 Uwanja wa Moi mjini Kisumu katika mchezo wa Nusu Fanali.

Msemaji wa TFF Clifford Ndimbo ameeleza kuwa, wakati wote Banka akitumikia adhabu hiyo hataruhusiwa kufanya chochote kinachohusiana na mpira wa Miguu, ikiwemo kufanya mazoezi hadharani au kuonekana akishiriki shughuli za mpira wa miguu.

Ndimbo ameongeza kuwa, mchezaji huyo alitakiwa kukutana na adhabu kubwa zaidi ikiwemo kufungiwa maisha lakini kamati kwa mamlaka iliyonayo imepunguza adhabu hiyo kufikia miezi 14 baada ya kumuona Mohamed Issa ni kijana mdogo.

Kwa upande wa Mohamed Issa amekiri na kujutia kitendo alichokifanya cha kutumia Bangi na ameahidi kuwa balozi mzuri kwa wengine wanaotumia dawa hizo zisizoruhusiwa michezoni.

Mnamo Disemba 9, 2017 Mchezaji huyo akiwa Machakos nchini Kenya alichukuliwa vipimo vya mkojo ambavyo vilisafirishwa kwenda kwenye Maabara ya WADA iliyopo Doha, Qatar kwa uchunguzi zaidi na majibu kurudi yakiwa na tuhuma hizo zinazomkabili.

Edinson Cavani kinara wa Golden Foot 2018
Watakaoivaa Bafana Bafana, Uganda watajwa