Meneja wa klabu ya Newcastle Utd, Rafa Benitez amefunga ukurasa wa kuwauza wachezaji wake kwa kusema inatosha na sasa anajiandaa na msimu mpya wa ligi daraja la kwanza nchini England (Sky Bet Championship).

Newcastle Utd, juma lililopita ilikubali kumuachia Andros Townsend aliyejiunga na klabu ya Crystal Palace na nafasi yake tayari imeshazibwa na  mshambuliaji Matt Ritchie aliyetokea  Bournemouth.

Ritchie amekua mchezaji watatu kusajiliwa na Benitez katika kipindi hiki baada ya kutanguliwa na mlinda mlango  Matz Sels pamoja na mshambuliaji Dwight Gayle.

Benitez amesema hatua hiyo inampa nafasi ya kuanza kujipanga vyema kwa msimu mpya wa ligi daraja la kwanza kwa kuamini wachezaji walionao kwa sasa watakidhi haja ya klabu ya Newcastle Utd, ambayo msimu uliopita ilikubali kushuka daraja ikitokea ligi kuu ya nchini England.

Amesema hatokubali kufanya biashara na yoyote atakayekuja kwa sasa, kutokana na wachezaji wote kuwa kwenye mipango yake ya kuhakikisha The Magpies inapambana na kufanikiwa kurejea ligi kuu msimu wa 2017-18.

“Nilijua kuna baadhi ya wachezaji wangeondoka na kujiunga na klabu nyingine katika kipindi hiki cha usajili, na imekua hivyo, lakini waliobaki nina mipango nao mikubwa ya kutimiza malengo yanayokusudiwa,” Alisema Benitez.

“Nina furaha ya kubaki na wachezaji waliopo kikosini, kutokana na kuamini wataweza kufanya kazi iliyo mbele yetu ya kupambana vizuri katika ligi daraja la kwanza na kisha tupate nafasi ya kuwa sehemu ya timu tatu zitakazopata nafasi ya kupanda daraja mwishoni mwa msimu.

“Nafahamu bado kuna baadhi ya klabu zinatolea macho Newcastle Utd kwa kutaka kuwasajili wachezaji nilionao kwa sasa, lakini niwafahamishe wahusika wa klabu hizo kwa kuwaambia kwamba, sitofanya biashara yoyote.” Alisisitiza Benitez

Meneja huyo kutoka nchini Hispania alikubali kuchukua nafasi ya Steve McClaren miezi miwili kabla ya kumalizika kwa ligi kuu msimu wa 2015-16 kwa misingi ya kutaka kunusuru jahazi la Newcastle Utd lisizame, lakini kwa bahati mbaya alishindwa kufikia lengo hilo.

Majuma mawili baada ya msimu kumalizika Benitez alikubali kuendelea na kazi ya kukinoa kikosi cha Newcastle Utd, huku akisisitiza kuwa na uhakika wa kuikamilisha hatua ya kurejesha heshima huko St James Park.

Cristiano Ronaldo: Siamini Kama Lionel Messi Amestaafu
Ugonjwa Usiojulikana Umeendelea Kuenea Dodoma na Manyara