Meneja wa klabu ya Newcastle Utd Rafael Benitez, amefunguka kuhusu mwenendo wa klabu hiyo upande wa usajili, kwa kusema hafurahishwi na kinachoendelea, wakati kikosi chake kikiwa kwenye maandalizi ya mwisho ya kuanza mshike mshike wa msimu mpya wa ligi kuu ya England.

Benitez tayari ameshafanikiwa kuwasajili baadhi ya wachezaji katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, lakini anaonyesha bado kuna mikakati mingine aliyojiwekea haijakamilishwa ipasavyo na viongozi wa juu ambao wanatakiwa kuidhinisha baadhi ya taratibu.

Miongoni mwa waliosajiliwa na meneja huyo kutoka nchini Hispania ni Jacob Murphy aliyetoka Norwich City kwa pauni milioni 12 na Florian Lejeune aliyetoka Eibar kwa pauni milioni 8.7.

Benitez ameiambia Sky Sports kuwa, bado kuna baadhi ya wachezaji aliowapendekeza hawajasajiliwa mpaka sasa, jambo ambalo anahisi huenda likakwamisha mipango yake katika mchezo wa ufunguzi dhidi ya Tottenham utakaochezwa siku ya jumapili.

“Sifurahishwi na kinachoendelea hapa, nilitarajia kuwa na wachezaji niliowapendekeza katika usajili, lakini mpaka sasa nimefanikiwa kupata wawili miongoni mwao, ninajaribu kufanikisha suala hili ili likamilishwe kabla ya dirisha kufungwa.” Amesema Benitez

Benitez amesema anatambua msimu wa ligi utakua mgumu kutokana na timu pinzani zilivyojiandaa, hivyo anaamini kama atafanikiwa kuwapata wachezaji aliowakusudia katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi, atakua amefikia malengo ya kabla ya msimu.

“Natambua sokoni kuna changamoto zake, lakini ipo haja kwa viongozi kupambana ili kufanikisha mpango wa kunikamilishia usajili wa wachezaji ninaowakusudia, lakini kama tutaendelea kuwa na kikosi nilichonacho sasa, hali itakua ngumu katika ushindani ninaoutarajia.” Aliongeza Benitez

Serikali yatoa onyo dhidi ya wananchi wanaouza ardhi
Alexis Sanchez Kuzikosa Leicester City, Stoke City