Aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Simba Alhaji Aden Rage amefafanua namna ambayo klabu hiyo inaweza kunufaika baada ya klabu ya Al Merrikh kuwatumia wachezaji waliofungiwa.

Simba SC imewasilisha malalamiko Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’ wakilalamika hatua ya Al Merrikh kuwatumia wachezaji wawili kinyume na sheria za usajili kwenye mchezo wa mzunguuko wa tatu wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya makundi, uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita mjini Khartoum, Sudan.

Rage amesema mchezaji hawezi kushiriki michuano ya Shirikisho la Soka Barani Afrika  kama hana leseni ya kushiriki ligi ya nchi anapocheza, hivyo ni dhahir madai ya Simba SC yanaweza kuwa na mashiko mbele kamati husika ya ‘CAF’.

“Timu ya Simba ina nafasi kubwa ya kupata alama tatu (3) kutoka kwa Al Merrikh. Wachezaji wawili wa Al Merrikh wamefungiwa na Chama cha Soka nchini Sudan baada ya kufanya kosa la kusaini klabu mbili tofauti makosa ambayo CAF na FIFA ni wakali sana.”

“Barua ambayo Chama cha Soka nchini Sudan kimeviandikia vilabu kuwajulisha wamewafungia wachezaji hao, kama wameomba baraka za CAF na FIFA, moja kwa moja wachezaji hao wanakosa sifa kucheza mashindano ya kikataifa.”

“Simba wanao mwanya mwingine wa kisheria wakiutumia nadhani watakuwa na nafasi ya kushinda rufaa yao. Ile adhabu ambayo wamepewa wachezaji wa Al Merrikh wamepoteza sifa ya kuwa wachezaji wa ligi ya Sudan.”

“Kwakuwa wamepoteza sifa ya kuwa wachezaji wa Sudan lakini sheria za CAF (Sheria namba 5 ya usajili) ili mchezaji aruhusiwe kushiriki mashindano ya CAF lazima awe na leseni ya kucheza mashindano ya ndani.” Amesema Rage.

Rage akaenda mbali zaidi kw akutoa mfano: “ Sasa wachezaji hao wamefutiwa leseni kushiriki mashindano ya ndani. Mfano Mohamed Mshangamo anacheza Kankunde FC, amefungiwa na TFF kucheza ligi lakini wakati huohuo Kankunde FC inacheza mashindano ya CAF na wanaamua kumchezesha Mohamed Mshangamo kuna mambo mawili.”

 1. Kama TFF hawatawaarifu CAF na FIFA kuhusu adhabu waliyompa Mohamed Mshangamo hakutakuwa na madhara yoyote.

 2. Kama CAF na FIFA wameidhinisha adhabu hiyo, Mohamed Mshangamo anakuwa kapoteza sifa.

“Mwanya mkubwa ambao Simba wanao ni kuuliza uhalali wa hizo kadi. Kama Sudan waliomba baraka za CAF na FIFA wachezaji hao wanakuwa wamepoteza sifa. Simba wanatakiwa kulalamikia kadi ambazo ilibidi zitumike tayari zilishafutwa kwa hiyo hawakuwa na uhalali wa kushiriki mashindano ya CAF.”

Metacha azua maswali Young Africans
PICHA: Baraza la Mawaziri SADC kukutana Machi 12-13